Saturday, October 13, 2012

WANAFUNZI 12 WAPOTEZA FAHAMU BAADA YA KUMPIGA PAKA


Wanafunzi 12 wa Shule ya Msingi Vingunguti jijini Dar es Salaam wameanguka na kupoteza fahamu kwa madai ya kishirikina ya kumpiga paka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio ambalo katika tetesi za awali ilidaiwa kuwa watoto tisa walikuwa wamekufa kutokana na kisanga hicho.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda huyo alikanusha taarifa za vifo na kuelezea kuwa kilichotokea kwa watoto hao ni kuanguka huku kila mmoja kabla ya kuanguka akipiga kelele na kutaja neno paka na baadaye kupoteza fahamu.

Alisema kisa cha mkasa huo ni asubuhi ya jana, ambapo wanafunzi waliokuwa wakicheza nje ya viwanja vya shule hiyo, walimuona paka juu ya paa la darasa moja la shule na kuanza kumpiga mawe.

“Kama kawaida ya watoto walipompiga paka yule alikimbia na wanafunzi wale waliingia darasani na kuendelea na masomo yao kama kawaida.”

Alisema ilipofika saa saba mchana wakati wa mapumziko, mmoja wa wanafunzi wa kike wa darasa la saba, alikwenda chooni lakini alisikika baadaye akipiga kelele huku akitaja jina la paka na baadaye kupoteza fahamu.

Alisema baada ya tukio hilo, wanafunzi wengine takribani 11 nao walikwenda chooni hapo na walikumbwa na mkasa kama wa mwanafunzi huyo kwani walipiga mayowe na kuanguka na kisha kupoteza fahamu.

Minangi alisema baada ya walimu wa shule hiyo kuona hali hiyo waliwataarifu wazazi wa wanafunzi hao ambao walifika shuleni hapo na kutaka kuanzisha vurugu huku wakitaka watoto wao kwa madai ya kutokuwepo kwa usalama shuleni hapo na mazingira ya kutatanisha.

“Hivyo walimu waliamua kupiga simu Polisi ambao walifika shuleni pale na kufanikiwa kuwatuliza wazazi wale na masomo kuendelea kama kawaida, hakuna madhara yoyote yaliyotokea,” alisisitiza.

Taarifa za awali zilizolifikia gazeti hili, zilidai kuwa watoto tisa wa shule hiyo walipoteza maisha baada ya kumpiga paka huyo huku wengine wakiwa hoi, jambo ambalo hata hivyo RPC huyo alilikanusha baadaye.


Source: Habari leo