MAUAJI ya mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten,
Daudi Mwangosi, na ya raia wengine yamezidi kuichafua Serikali ya
Tanzania, na sasa imefunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Uhalifu ya
Kimataifa (ICC) iliyoko The Hague, Uholanzi.
Mbali ya mashitaka hayo yaliyopelekwa huko tangu Septemba 28, mwaka huu, Tanzania pia imeshitakiwa kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Mashtaka
hayo yalifunguliwa na Kituo cha Haki za Binadamu, ambapo Mkurugenzi
Mtendaji wake, Hellen Kijo-Bisimba, alisema wamezitaka mamlaka hizo za
kimataifa kufanya uchunguzi na kuichukulia hatua stahiki za kisheria
Serikali ya Tanzania.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimechukua hatua hiyo kutokana na
kuongezeka kwa mauaji ya raia wakiwa katika mikono ya vyombo vya dola,
huku serikali ikigwaya kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.
Pamoja
na hatua ya kushtakiwa kwa serikali katika mamlaka hizo za dunia,
Bisimba alisema bado wanataka kuona viongozi wote wa serikali na vyombo
vya dola waliohusika kwa namna yoyote na mauaji ya Mwangosi na raia
wengine wakiwajibishwa.
Bisimba alisema hawaoni sababu za viongozi hao kutojiuzulu ama kuachishwa kazi na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Aidha,
mkurugenzi huyo aliitaka serikali kuacha propaganda zinazotaka
kuchochea vurugu katika taifa ambazo hazina tija na kutaka itambue kuwa
sasa ni wakati wa mfumo wa vyama vingi, hivyo ni vyema ikaacha kutumia
vyombo vya dola katika kuleta chuki na mafarakano katika jamii
yanayohatarisha usalama na amani ya Watanzania.
---
Ni sehemu ya habari kwenye gazeti la Tanzania Daima.
---
Sehemu ya habari kwenye gazeti la Mwananchi iliyoandikwa na Ibrahim Yamola na Raymond Kaminyoge inasema:
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC,
Dkt. Helen Kijo-Bisimba alisema kuanzia Januari hadi Septemba mwaka
huu, jumla ya watu 24 wameuawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na
usalama.
Dkt. Kijo-Bisimba Alisema:
“Tumepeleka
mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika
kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania
ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu,”
alisema Dkt. Bisimba.
“Tunatarajia kuona
uwajibikaji wa viongozi wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika
kwa njia yoyote ile. Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na
kujiuzulu, kuachishwa kazi na kufikishwa Mahakamani, ” alisema.
Taarifa
ya Kamati ya Dkt. Nchimbi... “LHRC hakijashangazwa sana pale taarifa
hiyo ilipoonyesha wazi nia ya kuwalinda watuhumiwa kwa kuwa Serikali
yetu bado haijajenga mfumo wa kujichunguza na kujiwajibisha
yenyewe.” “Serikali imeudhihirishia umma kuwa haikuwa na nia ya dhati ya
kuchunguza suala la mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, bali
ilikuwa na lengo la kulisafisha Jeshi la Polisi na kuwalinda maofisa
wake.”
Dk Bisimba
alisema tangu mwaka 2001 hadi sasa, kituo hicho kimekuwa kikifuatilia
kwa karibu matukio mbalimbali ya mauaji yanayoendelea kufanywa na vyombo
vya dola na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.
Kauli za Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawakili
Akizungumzia
suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema hana
taarifa za Serikali kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya The
Hague, “Kwa nini wameamua kutushtaki katika Mahakama ya The Hague? Kwani
hapa nchini hakuna mahakama au wameona ni bora wavuke mipaka... Kwa
sasa siwezi kulizungumzia zaidi suala hilo.”
Wakili
wa Kujitegemea, Gaudioz Ishengoma alipotakiwa kuzungumzia hilo alisema
anaunga mkono uamuzi wa kituo hicho kuipeleka Serikali kwenye Mahakama
ya Kimataifa.
Alisema
hilo ndilo eneo sahihi ambalo Serikali inatakiwa kupelekwa kwa sababu
ya ukiukaji wa haki za binadamu na kwamba huko ndiko ambako haki inaweza
kupatikana.
Hata
hivyo, Wakili mwingine wa Kujitegemea, Majura Magafu alipinga hatua hiyo
akisema kituo hicho kimekosea kuipeleka Serikali The Hague kwa kuwa
imekuwa ikichukua hatua za kisheria dhidi ya makosa mbalimbali ya mauaji
ambayo yamekuwa yakitokea, “Kwa mawazo yangu, hawa LHRC wamekosea
nadhani wamefanya hivyo kwa masilahi yao binafsi hasa ili kuonyesha
kwamba wanafanya kazi,” alisema.
Alisema
hata kama Serikali itakuwa imeshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi
ya wauaji, kituo hicho kilitakiwa kuishtaki Serikali katika mahakama za
hapa nchini, “Hawa sijui wanataka kutupeleka wapi kwa sababu wananchi
wengi wa Afrika
wakiwemo wa Kenya wamekuwa wakitaka mashtaka yasipelekwe nje ya nchi,
hivi kila kitu tunawategemea Wazungu kwa sababu gani hasa?”