Saturday, October 13, 2012

KITUO KIPYA CHA MABASI KUHAMISHIWA MBEZI LUIS

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki amesema ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani kinatarajiwa kujengwa eneo la  Mbezi Ruis.

Akizungumza na NIPASHE, alisema serikali imeanza mkakati wa kuwahamisha wakazi wa eneo hilo ili kupisha ujenzi wa kituo kipya cha mabasi kwani kituo cha Ubungo kinachotumika hivi sasa, kitatumika kwa ajili ya mabasi yaendayo kwa kasi (DART).

Alisema kwa mabasi yanayofanya safari zake ukanda wa Kaskazini yatajengewa kituo eneo la Boko na eneo la machimbo lililopo Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wao Chama Cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), baada ya kutishia kutohama katika Kituo cha Ubungo na kuunda tume ya watu watano ili kufikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa mkoa wamesema kuwa wamekubaliana na uamuzi huo wa Serikali baada ya kushirikishwa kuhusu ujenzi huo.

Aidha, Katibu wa chama hicho, Enea Mrutu, alisema baada ya kukutana na Mkuu wa Mkoa na kufafanuliwa juu ya suala hilo, chama kimeridhia ujenzi huo na hakutatokea vitisho vingine kuhusu kugoma kuhama Ubungo.

Hata hivyo, Mrutu alisema pamoja na kituo kipya kujengwa eneo husika, bado kutakuwepo na usumbufu mkubwa kwa wasafiri hasa wale waishio mbali na kituo hicho.


--
via gazeti la Nipashe