UTATA umegubika kuhusiana na kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni shilingi
milioni 700,000,000 zilizofichwa na Mary Mramba katika kabati nyumbani
kwake Stakishari eneo la Sabasaba, Ilala jijini Dar es Salaam.
Fumuafumua ambayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu sakata la fedha hizo
ambazo zilifichwa kati ya Novemba mwaka jana na Januari mwaka huu,
imegundua kwamba ziliibwa na watu kadhaa wakiwemo ndugu zake.
Imegundulika pia kuwa Mary alitoa taarifa Kituo cha Polisi Stakishari
Septemba mwaka huu na kufunguliwa jalada la kesi STK/RB/16109/2012 na
jalada la upelelezi STK/IR/12865/2012 akimtuhumu mtoto wa kaka yake
aitwaye Digna Mark na wenzake kuhusiana na kesi ya kughushi hati ya
nyumba na wizi huo.
Uchunguzi wa Fumuafumua umebaini kwamba mara baada ya Mary kugundua
mwezi Januari kuwa fedha hizo zilikuwa zimeibwa, hakutaka kupeleka
suala hilo polisi kwa sababu anazozijua yeye bali alifanya kikao na
wanandugu akiwemo Digna na kubaini tayari magari matano na nyumba mbili
zilizokuwa zinamilikiwa na mtu huyo ni vitu vilivyokuwa vimenunuliwa
kwa fedha hizo.
Alichokifanya Mary ni kumpigia magoti Digna arejeshee hayo magari na
nyumba hizo kwani hakutaka suala hilo alifikishe polisi. Pia
inasemekana hata ndugu zake wengine walitoroka na zaidi ya shilingi
milioni 400 kati ya fedha zilizoibwa. Imegundulika kuwa Digna aliiba
shilingi milioni 300 na zingine ziliibwa na ndugu zake na kutoweka nazo.
Mlalamikaji hakuwashitaki watu hao bali alikaa kimya ikidaiwa kwamba
angeshitaki angeulizwa alikozitoa fedha hizo nyingi.
Imebainika kwamba wanandugu hao waliamua kuiba fedha hizo wakiamini
Mary asingeweza kuwashitaki kutokana na kwamba wanajua jinsi fedha hizo
zilivyopatikana hivyo alihofia kuwa siri ingevuja. Taarifa zaidi
zinaeleza kwamba Mary aliamua mambo hayo yaishe kwa siri ndani ya
familia badala ya kupelekwa polisi ambapo yaliisha kwa upande wa Digna
kwani aliamua kurejesha mali alizonunua na fedha hizo alizochukua ambazo
ni shilingi milioni 300.
Hata hivyo, Mary alilazimika Septemba mwaka huu kwenda polisi baada ya
kusikia kwamba Digna ameenda huko kutoa taarifa kwamba hati ya nyumba
yake ilikuwa imepotea. Fumuafumua imegundua kuwa maelezo yaliyotolewa
na Mary huko polisi juu ya fedha hizo ni kuwa alitumiwa na ndugu yake
aitwaye Philipo Sindana aishiye nchini Italia kwa ajili ya kununua
nyumba, kitendo kinachopingwa na Digna ingawa hajawa tayari kuelezea
ukweli kwa sasa.
Hata hivyo, jalada la kesi hiyo liko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ili iandaliwe hati ya mashtaka. Wakati jalada hilo halijarudi, polisi
imeelezwa kwamba askari wa kituo hicho cha Stakishari walikuwa
wakilaumiana kwamba maelezo yalioandikwa hayakutosheleza na kuna kitu
kinafichwa. Fumuafumua imebaini kwamba jalada hilo limesharudishwa toka
kwa mwanasheria na kumweleza mkuu wa upelelezi Wilaya ya Ukonga, Idd
Kiogomo kwamba hamna kesi ya kumshtaki Digna juu ya wizi ama kughushi
bali ni kutoa taarifa za uongo za kupotelewa kwa hati ya nyumba.
Mkuu huyo wa upelelezi ameagizwa kutoa taarifa ya kina juu ya shitaka
la wizi kwani maelezo ya Mary yanaonyesha kwamba wizi ulifanyika
Januari hivyo iweje atoe taarifa hizo Septemba. Kiogomo ametakiwa
kuchunguza na kutoa maelezo juu ya upatikanaji wa fedha hizo nyingi na
kwa nini zilihifadhiwa ndani. Vilevile Mary aeleze ni mahakama gani
ilimpa kibali cha kutaifisha nyumba na magari ya Digna.
Kwa masaada wa Mtandao