Tuesday, October 23, 2012

POAC YAICHARUKIA MUHIMBILI;YATAKA IFUNGE OFISI ZA NMB

Habari imeandikwa na Halima Mlacha via HabariLeo

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imeutaka uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kulifunga jengo la ofisi ya benki ya NMB lililopo katika eneo la hospitali hiyo leo, kwa kuwa benki hiyo imepangisha kwa kampuni ambayo haimiliki jengo hilo.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto wakati alipokutana na menejimenti ya MNH kupitia hesabu za hospitali hiyo za 2010/2011, ambapo alisisitiza iwapo uongozi wa hospitali hiyo utashindwa, kamati itaenda kulifunga jengo hilo yenyewe.

Alisema jengo hilo lilijengwa na kampuni ya Regent Stores baada ya kuingia mkataba na Muhimbili mwaka 1987 kuwa baada ya miaka mitano, mali hiyo ikabidhiwe kwa hospitali hiyo lakini hadi mwaka huu ambao ni mwaka wa 20 liko mikononi mwa kampuni hiyo kinyume cha makubaliano.

“Ninavyofahamu mimi mkataba ulikuwa wazi kuwa baada ya miaka mitano, Regent Stores walitakiwa walirejeshe Muhimbili, lakini waligoma walipotakiwa kufanya hivyo mwaka 1992 kwa madai ya kuwepo kwa mkanganyiko wa tafsiri ya mkataba,” alisema Zitto.

Alisema pamoja na kwamba kampuni hiyo imefungua kesi mahakamani mwaka 2005 kupinga kuondolewa kwake katika eneo hilo mwaka 1992 kutokana na mkanganyiko wa mkataba, miaka imeenda na inatakiwa kuachia jengo hilo mikononi mwa hospitali hiyo sasa.

“Ila kinatushangaza kitu kimoja, huu ni takribani mwaka wa 20 sasa jengo hilo linashikiliwa kinyume na kampuni hii na wamelipangisha kwa benki ya NMB, nyinyi Muhimbili mlikuwa wapi? Au kuna kitu hapa? Sasa naagiza kesho (leo) mkatie kufuli jengo lile hadi kesi iishe si mali yao, ni ya Watanzania,” alisisitiza.

Alisema iwapo eneo hilo lenye ukubwa wa meta za mraba 400 litarejea mikononi mwa hospitali hiyo, litaongeza mapato kwa kuwa lipo sehemu nzuri na kutokana na gharama za sasa linaweza kuingiza dola za Marekani 7,200 kwa mwezi.

Pamoja na hayo, kamati hiyo iliagiza uongozi wa hospitali hiyo, kubadili mfumo wa kuhifadhi mafaili ya wagonjwa kwa kuwa malalamiko yanayoifikia kamati hiyo ni upatikanaji wa huduma kutokana na kupotea au kutoonekana kwa mafaili hayo.

Pia Zitto alihoji juu ya mfumo wa ununuzi wa dawa za Muhimbili kutoka Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) kuwa una mianya ya wizi kwa kuwa haufuati sheria na kanuni za ununuzi kutokana na MSD kujilipa yenyewe bila kusubiri kibali cha mzigo kupokewa kutoka Muhimbili.

Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alielezea kushangazwa na uongozi wa hospitali hiyo kuonekana kutokuwa na mori ya kurejesha jengo hilo mikononi mwake na kuachia kampuni hiyo ambayo si mmiliki halali ipangishe watu katika eneo hilo.

Mbunge wa Magomeni, Muhammad Amour Chomboh, alisema suala zima lina utata kwa kuwa haiwezekani kampuni hiyo ikampangisha mtu bila kuwa na hati ya umiliki na kuhoji huenda jengo hilo limeuzwa kinyemela.

Hata hivyo wakili wa hospitali hiyo, Veronica Hellar, alikanusha kwamba jengo hilo limeuzwa na kusisitiza kuwa bado ni mali ya Muhimbili na kwamba kwa sasa kuna kesi ya mkanganyiko wa tafsiri ya mkataba iliyofunguliwa na kampuni hiyo katika Mahakama ya Ardhi na inaendelea vizuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Marina Njeleka, alikiri kuwepo kwa tatizo la mfumo wa kuhifadhi mafaili hospitalini hapo na kwamba kwa mwaka wa fedha 2012/2013 wamepanga kuubadili na kuwa wa kieletroniki lakini zinahitajika Sh milioni 790.