Habari hii ni kwa mujibu wa Fadhili Abdallah, HabariLeo, Kigoma ---
POLISI mkoani Kigoma wamewapa kipigo mahabusu kutoka Gereza la Bangwe
mjini Kigoma waliogoma kushuka kwenye karandinga, hivyo kusababisha
vurugu kubwa kwenye Mahakama ya Mkoa mjini hapa.
Kutokana
na kipigo hicho, mahabusu Maneno Kichako alipigwa na kuumizwa na
hatimaye kupoteza fahamu hivyo kukimbizwa Hospitali ya Mkoa ya Maweni
kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, Fraiser Kashai amekiri kuwapo kwa vurugu hizo, na kuongeza kuwa
kwa taarifa alizonazo, mahabusu huyo hakuumia kutokana na kipigo cha
askari, bali alianguka kutoka kwenye ngazi za karandinga lenye namba STH
2929 lililowachukua kutoka mahabusu ya Bangwe mjini hapa.
Awali
mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa baada ya karandinga la Polisi
kuwasili mahakamani hapo, mahabusu hao waligoma kushuka na badala yake
walianza kupiga kelele huku wakifunga mlango wa kutokea katika gari hilo
ili kuzuia askari kushindwa kuwashusha.
Hali
hiyo iliwalazimu askari walioongozana na gari hilo kulipeleka Kituo
Kikuu cha Polisi mjini Kigoma na hapo walianza kupewa kipigo ili
kuwafanya kulainika na kuruhusu ratiba ya siku kuendelea.
Kutokana
na fujo walizofanya mahakamani, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi ya Mkoa, Emanuel Mrangu amewahukumu kifungo cha miezi sita
mahabusu watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya mauaji, kwa kufanya fujo
wakilalamika kesi yao kuchukua muda mrefu bila kutolewa hukumu.
Waliohukumiwa
kifungo hicho ni Maneno Kichako, Majuto Dunia na Haruni Petro ambao
inadaiwa walikuwa vinara wa mgomo wa kushuka na kufanya fujo
wakishinikiza wenzao kutoingia mahakamani.
Mrangu
aliwahukumu kifungo hicho cha miezi sita jela watuhumiwa hao kwa kosa
la kufanya fujo mahakamani na kusema kuwa kama walikuwa na madai yao
kuhusu kucheleweshwa kwa mwenendo wa kesi zao, walipaswa wapeleke
malalamiko hayo kwa kufuata taratibu za kimahakama, lakini si kufanya
fujo mahakamani na hivyo kesi mbalimbali zilizokuwa zikiendeshwa
kusimama kwa muda.
Aidha, Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mrangu alisema amewasiliana na uongozi wa Magereza Mkoa kuona
namna gani suala kama hilo linapatiwa ufumbuzi ikiwamo mchakato wa kesi
kuchukua muda mrefu huku akitoa angalizo la kuwataka maofisa Magereza
kuandika barua za maombi wa mwenendo wa kesi kukumbusha kushughulikiwa
kwa kesi ambazo zimechukua muda mrefu bila kumalizika