Katika Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mahesabu za Mashirika ya UMMA (POAC)
mnamo tarehe 24/10/2012 Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt. Ramadhani K. Dau
akijibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge alitoa maelezo ya msingi kuhusu
umuhimu na dhana kamili ya Hifadhi ya Jamii.
Katika maelezo hayo
alifafanua kuhusu madhara ya kujitoa kwenye mfuko kwa mwanachama aliye
na uwezo wa kuendelea na kazi, na alisisitiza kuwa madhara ni kwa
Mwanachama zaidi kuliko kwa Mfuko. Dkt.Dau alifafanua kuwa uamuzi wa
kusitisha kwa Mafao ya kujitoa hauna uhusiano wowote na hali ya sasa ya
kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Dkt. Dau aliieleza Kamati
ya Bunge kuwa hali ya kifedha ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hupimwa kwa
kufanya Actuarial Valuation. Kwa upande wa NSSF zoezi hilo limefanywa
mwaka 2009 na Kampuni kutoka Canada iliyoteuliwa na ILO na mwaka 2010 na
Kampuni kutoka Afrika Kusini iliyoteuliwa na SSRA.
Matokeo
yameonyesha kuwa NSSF HAINA MATATIZO YA KIFEDHA kwa sababu ina uwezo wa
kuwalipa Wanachama wake na kulipia gharama za uendeshaji kwa kipindi cha
miaka 50 ijayo bila kutetereka.
Dkt. Dau alifafanua zaidi
kuhusu kutokuwepo kwa mafao ya kujitoa katika mfumo mzima wa Pensheni
ulimwenguni kwa muongozo wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 102 wa
mwaka 1952 [The ILO Social Security (Minimum Standards) Convention, 1952
No. 102] ambao ndio unatoa maelekezo ya jumla kuhusu Sekta ya Hifadhi
ya Jamii ulimwenguni kote.
Katika Muongozo huu ILO imetamka wazi
kuwa kuna aina tisa (9) za mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii na katika hayo hakuna mafao ya kujitoa. HITIMISHO Tunapenda
kuwataarifu Wanachama na Wananchi kwa ujumla kuwa majibu haya ndio
yaliyotolewa katika Kamati ya Bunge.
Taarifa zilizotolewa na
baadhi ya Vyombo vya Habari kuwa “Mkurugenzi Mkuu wa NSSF apinga Mafao
ya Kujitoa” zimetolewa nje ya maudhui yaani “Out of Context” Suala la
Mafao ya kujitoa (Withdrawal Benefit) linashughulikiwa na Serikali na
iwapo itaamuliwa na Bunge kurudisha mafao hayo,
NSSF HAINA PINGAMIZI na uamuzi huo na italipa mafao hayo bila wasiwasi wowote kwani ina uwezo mkubwa wa kifedha.
IMETOLEWA NA IDARA YA UHUSIANO - NSSF