Saturday, October 27, 2012

MASHIRIKA 70 YANAJIENDESHA KWA HASARA NCHINI TANZANIA POAC YAAGIZA KUTATHIMINIWA

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeliagiza Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), kuyafanyia tathmini mashirika yote ya umma, ili kufahamu hasara inayopatikana, kwa kuwa mashirika 70 yanajiendesha kwa hasara.

Pamoja na hayo, alisema Serikali inatakiwa kueleza ina hisa kiasi gani katika mashirika hayo.

Agizo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, wakati kamati yake ilipokutana na Bodi ya CHC, kwa ajili ya kupitia hesabu za shirika hilo.

Alisema kwamba, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha linayafanyia tathmini mashirika yote ambayo ina hisa, ili CHC ipewe mtaji wa kutosha, kwa ajili ya kutekeleza agizo hilo.

Pamoja na hayo, alisema kamati hiyo ya Bunge inataka sheria zilizowekwa zifuatwe, ili msajili wa hazina asiwe mjumbe wa bodi ya CHC.

Pia kamati hiyo, iliiagiza CHC isiuze jengo la Joji's grill maarufu kama NBC Klabu, lililopo nyuma ya Benki ya NMB, Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na kutaka mchakato ufanyike, ili kuhakikisha zinapelekwa taarifa mahakamani, ili kesi iliyofunguliwa dhidi ya klabu hiyo, imalizike," alisema.

Awali, akielezea namna ambavyo mashirika 70 yanaendeshwa kwa hasara, Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, Dkt. Marcellina Chijoriga, alisema mashirika hayo ni yale ambayo yamebinafsishwa katika mpango maalum wa kubinafsisha mashirika ya umma.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto nyingi, yapo mashirika ambayo yamebinasfishwa, lakini yanaendeshwa kwa hasara,” alisema Dkt. Marcellina.

Aliyataja mashirika hayo kuwa ni mashirika ya kilimo 33, mashirika ya viwanda na biashara 24 na Maliasili na Utalii, mashirika 13.

Wakati huo huo, alisema maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo yatafanyiwa kazi, ili ufanisi uwepo.

---
via MTANZANIA