Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini mkoani
Tanga, Annah Mwahalende, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi na tuhuma
zinazomkabili.
Kwa
mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata na kuthibitishwa na viongozi
wa mkoa wa Tanga, mkurugenzi huyo na barua za kusimamishwa kwake
zimepelekwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Chanzo
cha habari kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kinaeleza kuwa
Mkurugenzi huyo alikabidhiwa barua hiyo Oktoba 24, mwaka huu mjini
Korogwe.
Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia,
akizungumza na gazeti la NIPASHE, alisema suala hilo ni la kiutendaji
zaidi hivyo wizara iachwe ifanye kazi yake.
“Suala
la kusimamishwa Mkurugenzi ni la kiutendaji zaidi, mtuachie tufanye
kazi maana hiyo wilaya ya Korogwe Vijijini ilikuwa imeachwa watu
wanafanya kazi kienyeji zaidi,” alisema Ghasia.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Monika Kinala, alithibitisha kuwepo kwa
barua ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi hiyo iliyotoka TAMISEMI.
“Barua
ipo, lakini mimi siyo msemaji wa suala hilo, watafute wahusika au
wasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe atakweleza,” alisema Kinala.
---
via Nipashe