Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi jana alipanda kizimbani
katika kesi ya wizi wa kuaminika wa Sh milioni 37.4 inayomkabili
Abdallah Mzombe (39), ambaye alikuwa mfanyakazi wake huku wanahabari
wakizuiwa kusikiliza.
Mzombe alifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Agosti 21 akidaiwa kuwa
katika siku tofauti kati ya Januari mosi na Julai 10, akiwa wakala wa
kukusanya kodi kwenye nyumba za Mzee Mwinyi, aliiba Sh milioni 17.6.
Inadaiwa
aliiba fedha hizo za kodi ya mwaka 2011/12 na 2012/13 alizokuwa
amekusanya kutoka kwa mpangaji wa nyumba namba 481 ya Mikocheni.
Katika
mashitaka mengine, Mzombe anadaiwa kuiba Sh milioni 19.8 za malipo ya
kodi ya mwaka 2011/12 na 2012/13 ya mpangaji wa nyumba namba 55 ya
Msasani Village.
Hakimu Gane Dudu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22 kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na mshitakiwa alirudishwa rumande.
Katika
hali isiyo ya kawaida, walinzi wa Mzee Mwinyi walizuia waandishi wa
habari kuingia mahakamani kusikiliza ushahidi aliokuwa akiutoa na Rais
huyo mstaafu.
Mwinyi alifika mahakamani hapo na
kuingia kwenye chumba cha Mahakama saa 5 asubuhi, lakini walinzi wanne
walizuia waandishi kuingia kwenye chumba cha Mahakama.
Kabla
ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, walinzi hao walionekana wakizunguka
eneo la Mahakama na muda ulipofika, walisimama mlangoni na kuzuia
waandishi kwa madai kuwa kesi hiyo haiwahusu.
Mahojiano kati ya walinzi hao yalikuwa kama ifuatavyo:
Mlinzi: Mnakwenda wapi?
Waandishi: Tunaingia mahakamani
Mlinzi: Ninyi ni akina nani na mmeambiwa kuna Mahakama humu?
Waandishi: Sisi ni waandishi wa habari na hii ni Mahakama.
Mlinzi
mwingine akasema: "Msiingie huku kesi hii haiwahusu" na kuweka mkono
kwenye mlango wa chumba cha Mahakama kuzuia waandishi.
Mwinyi
alimaliza kutoa ushahidi na kutoka kupitia mlango wa nyuma wa Mahakama
saa 6.21 mchana na kuchukuliwa na gari namba T 914 BJT aina ya Toyota
Land Cruiser lenye vioo vyeusi.
Mzee Mwinyi anakuwa
Rais mstaafu wa pili kutinga mahakamani kutoa ushahidi katika kesi.
Kabla yake, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alifika
mahakamani hapo kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa
ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa
Mahalu.
Tofauti ya kesi hizo mbili; Mwinyi yeye
amekwenda kutoa ushahidi katika kesi inayomhusu yeye binafsi na
iliyotokea wakati akiwa amestaafu, wakati Mkapa alikwenda kutoa ushahidi
katika kesi iliyohusu utendaji wake akiwa Rais.
---
Habari via gazeti la HabariLeo