Tuesday, October 9, 2012

MKUU WA MKOA AAMURU WANAFUNZI WALIAOCHISHWA KUFANYA MTIHANI WAFANYE MTIHANI

Habari imeandikwa na Woinde Shizza via via blog -- Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mullongo jana alifanikiwa kuzima jaribio la mkuu wa shule ya sekondari Peace house iliyopo eneo la Kisongo jijini Arusha la kumzuia kutofanya mtihani wa kidato cha nne mwanafunzi, Willbard Moshi aliyekuwa amefukuzwa kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Mulongo alimwamuru mkuu wa shule hiyo Christopher Mushi, kumruhusu mwanafunzi huyo kufanya mtihani bila masharti yoyote na kumweleza kuwa huo sio mtihani wa shule hiyo bali ni mtihani wa taifa na ni haki ya msingi kwa mwanafunzi kuufanya.

Alieleza kuwa kitendo cha uongozi wa shule yeyote kumzuia mwanafunzi kufanya mtihan iwa taifa ni kosa kisheria na kwamba mhusika anapaswa kuchukuliwa hatua kali kwani makosa ya mwanafunzi hayahusiani na mtihani wa taifa na ukizingatia barua ya kufukuzwa alipatiwa siku moja kabla ya mtihani, ‘Hairuhusiwi kumsuia mwanafunzi kufanya mtihani labda kama alifukuzwa muda mrefu haliwezekani lazima mwanafunzi huyo afanye mtihani kwa hiyo nakuagiza mwalimu mkuu mruhusu mwanafunzi afanye mtihani bila masharti yoyote’’alisema Mulongo.

Akizungumza shuleni hapo, Mkuu wa Shule hiyo alidai kuwa mwanafunzi huyo hakupaswa kufanya mtihani akidai kuwa bodi ya shule hiyo iliridhia kutimuliwa kwake kutokana na makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu likiwemo la kukutwa na mwanafunzi wa kike kwenye bweni.

Mkuu huyo aliongeza kuwa kosa jingine , mwanafunzi huyo aliruka uzio wa shule na kutoroka katika kipindi cha Sensa hata hivyo alikiri kwamba uongozi wa shule hiyo haukuwahi kumpatia barua ya onyo ama karipio la mdomo hadi agosti 7 siku moja kabla ya mtihani wa kidato cha nne, ilipompatia barua ya kumfukuza shule.

Naye mlezi wa mwanafunzi huyo, Hadija Juma alipiga kitendo cha mkuu wa shule hiyo kumzuia mtoto huyo kufanya mtihani akidai kuwa maamuzi hayo hayakuzingatia sheria na kwamba yalilenga kumkomoa na kupoteza mwelekeo wa misha ya mwanafunzi huyo.

Alisema yeye kama mlezi wa mtoto huyo hakuwahi hata siku moja kuitwa na uongozi wa shule na kufahamisha mwenendo wa mtoto huyo, na siku zote amekuwa akishirikiana vema na mkuu wa shule hiyo ila alishtushwa sana kupata barua ya kufukuzwa shule kwa mtoto wake na kuamuriwa kutofanya mtihani wa kidato cha nne ulionza nchini kote oktoba 8 .

Aliongeza kuwa baada ya kupata barua hiyo aliamka alfajiri na kwenda shuleni hapo akiwa na mwanafunzi huyo kwaa lengo la kuonana na mkuu wa shule hiyo, hata hivyo mkuu huyo alitoa agizo kwa kuwataka walinzi la shule kumzuia mtu yoyote kuingia ndani ya shule hiyo.

Alisema kitendo hicho kilimchangaza sana na kuamua kutoa taarifa kwa mwandishi wa habari hizi ambaye alifika shuleni hapo kwa lengo la kupata taarifa kamili juu ya kumzuiwa kwa mwanafunzi huyo kufanya mtihani.

Baada ya maelezo ya mkuu wa shule, mwandishi wa habari hizi aliwaasiliana kwa njia ya simu na mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na baada ya kuelezwa taarifa hiyo aliamuru kwa kumtaka mkuu wa shule hiyo kumruhusu mwanafunzi huyo afanye mtihani huo bila masharti yoyote, ambapo mwanafunzi huyo aliyekuwa tayari amefanikiwa kujipenyeza na kuingia ndani ya chumba cha mtihani aliendelea kufanya mtihani huo.