Habari imeandikwa na Pascal Michael, Rorya
MKAZI mmoja wa Kijiji
cha Kogaja kata ya Goribe wilayani Rorya mkoani Mara Bw. Hamisi Omenda
(33) amedaiwa kumuua kikatili mke wake Bi. Levina Hamisi (27) kwa
kumkatakata kwa panga na kisha kutoroka, huku Polisi wakidaiwa kushiriki
katika utoro huo kwa kuandaa mazingira ya kutoroka.
Polisi wa
kituo cha Kogaja wanadaiwa kuhusika na utoro huo kwa kile kilichodaiwa
kuwa hawakumkamata mtuhumiwa licha kufika kituoni hapo kuchukua PF3
baada ya kufanya kitendo hicho.
Hata hivyo, taarifa kutoka Kituo
cha Polisi Kogaja zimedai kuwa Mtuhumiwa alitoa maelezo kuwa mkewe
alikatwakatwa mapanga na watu wasiofahamika hivyo aliomba PF3 kwa ajili
ya kumpeleka marehemu katika Hospitali ya Tarime mjini Tarime.
Utetezi huo unadaiwa kuwa ni njama ya Polisi kwa kuwa wanayo mahusiano wa kibiashara na mtuhumiwa huyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mtendaji wa Kijiji cha Kogaja, Bw. Lukas
Ambonya alikiri Bw. Omenda kuhusika katika tukio hilo na kwamba wakiwa
njiani kwenda hospitalini mke wake alifariki na yeye kutokomea
kusikojulikana hivyo hakuwepo hata wakati wa maziko.
Kitendo
hicho kiliwakasirisha ndugu wa marehemu ambapo juzi wakati wa maziko
walitishia kuvamia kituo cha Polisi na kutaka kuchoma baadhi ya nyumba
za ndugu wa mtuhumiwa kijijini hapo.
Alisema chanzo cha mauaji
hayo ni marehemu kutofautiana na Mumewe siku ya Jumamosi asubuhi, tarehe
20 Oktoba, 2012, (tofauti ambayo haijawekwa bayana), na marehemu baada
ya kuhisi hali ya hatari alikimbia kutoka nyumbani hapo.
Hata
hivyo mume wake Bw. Omenda aliwatuma baadhi ya vijana kwa pikipiki
waolifanikiwa kumkamata na kumrudidha nyumbani ambapo majira ya saa 4
asubuhi siku hiyo alimfungia ndani na kuanza kumkatakata kwa panga.
“Sisi
tunasema haya kwa sababu tunaishi kijijini hapa na Bwana huyu ana
mahusiano makubwa na polisi hawa , ndio maana hawakutaka kumtia ndani
badala yake walisaidia kuandaa njama za kutoroka kwake ..yeye alipeleka
mke wake hospitalini akiwa marehemu” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka
kutaja jina.
Marehemu hajaacha watoto.
Polisi inawashikilia baadhi ya ndugu wa mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi.
---
Imewasilishwa na Magiri Paul wa wotepamoja.com