Napenda kutumia fursa hii kuwapa
taarifa kuhusu tukio la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barlow yaliyofanywa na
watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo tarehe
13/10/2012 majira ya saa saba usiku Mkoani Mwanza.
2. Tukio hilo limetokea wakati
kamanda huyo akitokea kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la
Frolida hotel Mwanza mjini, akiwa na ndugu yake waliyeongozana nae
kutoka kwenye kikao hicho. Wakati akimshusha huyo ndugu yake eneo la
Kitangiri Minazi Mitatu, walitokea watu wanaosadikika kuwa ni majambazi,
na kumvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi na kumuua papohapo.
3. Ndugu wananchi, kufuatia tukio
hilo, tayari nimemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI
Robert Manumba kwenda mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na
upepelezi wa tukio hilo.
4. Najua tukio hili limetushitua
na kutuhuzunisha wote. Hivyo, wakati tukiendelea na taratibu zingine
kuhusiana na tukio hilo, niwaombe wananchi wote kuwa watulivu na kutoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao.
5. Tutaendelea kuwapa taarifa za tukio hilo, kadri tutakavyoendelea kuzipata.