MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na
kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa
kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.
Awali,
ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa
kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani
kwake, alivamiwa na majambazi. Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI,
Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina
tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja amekamatwa, lakini kwa sasa
siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado tunamhoji
na tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.”
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo
kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya
kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo
siwezi kuzungumzia lolote.”
Habari za
uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba upelelezi wa
mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo alikamatwa
Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo katika timu
ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako anashikiliwa na jeshi
hilo.
Ilielezwa kuwa mtu huyo
alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia
kutoka kwa watu mbalimbali, “Kuna hali imefunguka na imesaidia sana.
Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa
akifika nyumbani kwake, kama mumewe na watu wanajua jambo hili,”
alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini.
Alisema kwamba uchunguzi wa
awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa
mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha mauaji hayo lengo likiwa ni
kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano,
“Mimi natambua kwamba huyu
jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke
wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo kwani walishagombana siku moja mjini
na hata katika msiba nyumbani kwao na mtuhumiwa,” alisema mama mmoja
(jina tunalo), aliyejitambulisha kama mmoja wa marafiki wa karibu wa
Dorothy.
Mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa
aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila mara amekuwa akimkuta
hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi wenzake.
“Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.”
Dorothy
ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana
na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest Lyimo mwaka
1997.
“Watu wote wanajua kwamba
mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo mwalimu, wameonekana mara nyingi
wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa karibu wa mke wa mtuhumiwa.
Hili
ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa.
Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari aliyetambulika kwa
jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni
majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka 1997, aliyekuwa
Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la
Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi waliokuwa
wakijitayarisha kuvamia.
Dar wamuaga Kamanda Barlow
Makamu
wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza waombolezaji waliofika kutoa
heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Barlow nyumbani kwake, Ukonga
Dar es Salaam jana.
Mwili wa Kamanda
Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi,
uliwasili nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya kupelekwa katika Kanisa la
Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada na kutoa heshima za
mwisho.
Akitoa salamu za Serikali,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema kifo cha
Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa... “Tutahakikisha watuhumiwa
wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua za kisheria zinachukuliwa
dhidi yao.”
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi.
“Kifo
cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa askari mmoja analinda
watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la aina gani na
ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema IGP Mwema.
Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu.
Akitoa
mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea kwa wakati na kifo
cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye mamlaka ya
kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo chake siku
ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo.
IGP
Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda Barlow kwa uchapaji
wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi
kwa weledi uliotukuka.
“Daima nitamkumbuka kwani nimefanya naye kazi
sehemu tofauti na askari waliobaki waige mfano wake wa uwajibikaji”
alisema Mahita.
Mbali ya Dk Bilal,
viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo jana ni Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya
siasa na wananchi.
---
Habari hii imeandikwa na Frederick Katulanda (Mwanza); Ibrahim Yamola (Dar es Salaam) via hgazeti la Mwananchi