Friday, September 21, 2012

YANGA YAMTIMUA KOCHA WAKE MPYA

YANGA imemtimua kocha wake Mbelgiji, Tom Saintfiet baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa siku 80 kamili.

Saintfiet amefukuzwa usiku huu, baada ya kutofautiana sera na uongozi wa Yanga na sasa Fredy Felix Minziro, aliyekuwa Msaidizi wake, atakaimu nafasi yake.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb, amethibitisha kufukuzwa kwa Mbelgiji huyo ambaye ameiongoza Yanga katika mechi 14, kushinda 11, vipigo viwili na sare 1.

Habari zaidi, kuhusu kufukuzwa kwa kocha huyo, Yanga itatoa taarifa rasmi kesho asubuhi saa 3:00, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani. 

Saintfiet aliyetua nchini Jumatano, Julai 4, 2012 na kuirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic, amefukuzwa siku moja tu baada ya kuwatuhumu wachezaji kuwa "masharobaro" kama moja ya sababu za mwanzo mbaya wa msimu kwa timu hiyo ambayo inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa timu 14 za Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 1 kutokana na mechi mbili - sare ya 0-0 dhidi ya Prisons Jumamisi na kipigo cha aibu ambacho hakikutarajiwa cha 3-0 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Kabla ya kuwatuhumu wachezaji kwa kujiona mastaa wakubwa na kubadili mitindo ya nywele kila baada ya siku tatu ili kupamba kurasa za magazeti, Mbelgiji huyo alianika jinsi walivyolazwa wawili wawili mjini Mbeya wakati walipoenda kucheza dhidi ya Prisons katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Alilalamikia wachezaji kucheleweshewa chakula na wenye hoteli na kwamba alilazimika kuoga kwa kutumia kopo kutokana na mabomba ya 'mvua' ya kutotoa maji.

REKODI YA SAINTFIET YANGA

  1. Yanga Vs JKT Ruvu  (Kirafiki)                   2-0
  2. Yanga Vs Atletico (Burundi, Kagame)          0-2
  3. Yanga Vs Waw Salam (Sudan, Kagame)      7-1
  4. Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)              2-0
  5. Yanga Vs Mafunzo (Z’bar, Kagame)         1-1  (5-3 penati)
  6. Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)             1-0
  7. Yanga Vs Azam (Kagame)                         2-0
  8. Yanga Vs African Lyon (Kirafiki)               4-0
  9. Yanga Vs Rayon (Kirafiki, Rwanda)           2-0
  10. Yanga Vs Polisi (Kirafiiki, Rwanda)            2-1
  11. Yanga Vs Coastal Union    (Kirafiki)           2-1
  12. Yanga Vs Moro United      (Kirafiki)          4-0
  13. Yanga Vs Prisons    (Ligi Kuu)                  0-0
  14. Yanga Vs Mtibwa (Ligi Kuu)                     0-3
Picha, maelezo: Blogu za Staika Mkali & BongoStaz