Rais Kikwete akiweka jiwe la msingi kuashiria kuzindua rasmi ujenzi wa
Daraja la Kigamboni katika hafla iliyofanyika huko Kurasini jijini Dar
es Salaam leo mchana. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi Dkt. Magufuli na wa
pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt. Ramadhani Dau. NSSF
itagharamia asilimia 60 za ujenzi wa daraja hilo na Serikali asilimia
40. (Picha: Freddy Maro/IKULU)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa
Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao amewaeleza
kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza
nguvu kwenye maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia
wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili
ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa
watalipwa stahili na haki zao zote.
Daraja hilo la Kigamboni
ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya kwanza zaidi ya
miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 214.6 na litakuwa
tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo unaweza kupungua
na kubakia miezi 30.
Daraja hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita
680 linagharimiwa kwa pamoja na Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii
la NSSF ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60 na Serikali asilimia
40.
Daraja hilo ambalo litakuwa na jumla ya barabara za kupitisha
magari sita kwa wakati mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China
ambayo ni China Railway Construction Engineering Group na China Railway
Major Bridge Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni
Kampuni ya Misri.
Daraja hilo litapunguza adha ya usafiri kati ya
Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa sasa unategemea vivuko, ama boti
ndogo, mitumbwi ama wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita
52. Kwa uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum
kwenye daraja hilo pamoja na waendesha baiskeli watavuka bure bila
malipo yoyote.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete
amesema kuwa Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote
ambao wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya
wa Kigamboni watalipwa haki na stahiki zao. Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama
kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.
Rais Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya suala la kutunga na kusema uongo kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu
wana viwanda vya kuzalisha uongo. Wanashinda wanasambaza uongo kwenye
mitandao, kila mahali. Wamepata hata kusema kuwa mimi nimemuuzia George
Bush eneo la Kigamboni. Bush aje kufanya nini Kigamboni?”
Rais pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi maendeleo ya nchi. “Wanatamani
kila siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini watakufa kwa
kihoro kwa sababu hatutashindwa. Kila tulilosema tutalifanya,
litafanyika”.
Amesema kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi. “Lakini
wapo wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda hata daraja
hili lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa ni
kuweka maslahi yetu sote mbele.”
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Dar es Salaam. 20 Septemba, 2012
|