Tuesday, September 25, 2012

MUHIMBILI SASA KUTOA MAFUNZO YA MFUMO WA CHAKULA

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutoa huduma ya tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula baada ya kuwasili vifaa na vyombo maalumu kwa ajili ya huduma hiyo.

Mbali na vifaa hivyo, pia kimeanzishwa kitengo cha mafunzo na tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula Afrika Mashariki na tayari kitengo hicho kimeanza kutoa elimu ya juu kwa wataalamu wa tiba hiyo wakiwemo madaktari na wauguzi 40 kutoka hospitali za mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Marina Njelekela akifungua warsha ya mafunzo kwa wataalamu wa tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula, alisema juhudi kubwa zimefanyika kuanzisha mradi huo na kwamba moja ya mafanikio hayo ni kufika kwa vifaa na miundombinu kwa ajili ya kitengo hicho.

Dkt. Njelekela alisema lengo la kitengo hicho ni kujenga uwezo wa kutoa mafunzo na tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula katika hali ya ubora na kitaalamu zaidi nchini na Afrika Mashariki.

Dkt. Njelekela alishukuru Taasisi ya Ujerumani kwa kuwezesha kifedha na vifaa kwa ajili ya kitengo hicho pamoja na Profesa Rudolf Arnold kutoka taasisi hiyo kwa kufika nchini kufanikisha uzinduzi wa mafunzo hayo.

Alisema hiyo ni changamoto kwa watumiaji na wakufunzi kuhakikisha wanalinda na kutunza vifaa hivyo kwa kufuata taratibu za matumizi yake ili kuepusha kuvunjika na kuviharibu.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo ya tiba na huduma ya magonjwa ya mfumo wa chakula, Dkt. John Rwegesha alisema kitengo hicho kimeanza rasmi kutoa elimu ya juu ya tiba ya magonjwa hayo kwa madaktari na wauguzi na kwamba vyombo vya huduma hiyo tayari vimefika na katika kipindi cha miezi mitatu vifaa vyote vitakuwa vimewasili.

Dkt. Rwegesha alisema vile vile Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba (MUHAS) kinaanzisha Shahada ya mfumo wa tumbo na matarajio yao kitengo kipya cha mafunzo na tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula kitakuwa bora Tanzania na Afrika Mashariki.