Tuesday, September 25, 2012

MWALIMU AWEKWA NDANI MIAKA MITATU KWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

Hussein Semdoe, MWANCHI, Handeni -- MWALIMU wa Shule ya Msingi Magamba, wilayani Handeni,  amehukumiwa kutumikia kifungo  cha miaka mitatu jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mapenzi na kumpa mimba mwanafunzi.

Mwalimu huyo, Daniel Lukindo (24), alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumpa mimba mwanafunzi Halima Rashidi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kwaluguru.

Akisoma mashitaka katika shauri hilo  namba 240 la mwaka huu, Mwendesha mashitaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Elibaliki Polangyo, alieleza mahakama kuwa kati ya Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu katika Kijiji cha Magamba, mwalimu Lukindo alikuwa akifanya mapenzi na mwanafunzi huyo na baadaye, kumpa ujauzito.

Katika kesi hiyo iliyokuwa chini ya  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Handeni, Patrick Maligana, mshtakiwa alikiri kosa lake, akikubaliana na maelezo yote yaliotolewa na mwendesha mashitaka. Kufuatia hatua hiyo, Hakimu Maligana, alimtia hatiani na kumhukumu kutumikia adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Akifafanua kuhusu adhabu hiyo, Maligana alisema mshtakiwa alitenda kosa baya na hasa ikizingatiwa kwamba ni mwalimu anayepaswa kuwa mfano mzuri katika jamii, kwa kuzuia na kukomesha wimbi la matukio ya wanafunzi wa kike kupata mimba.

“Sheria inasema mwanaume yeyote atakayempa mimba mwanafunzi atakuwa ametenda kosa na kama atapatikana na hatia, atastahili kutumikia kifungo kisichopungua miaka mitatu jela na kisichozidi miaka sita. Kosa hili halitakuwa na nafasi ya kulipa faini,” alisema Maligana.

Alisisitiza kwamba adhabu hiyo alitoa itakuwa fundisho kwa walimu na wanaume wengine wenye tabia ya kupenda kufanya mapenzi na wanafunzi wa kike.