WANANCHI wa kata tatu za Wilaya ya Moshi Vijijini, wamekumbwa na hofu
kubwa inayofuatia kuibuka kwa vitendo vya ujambazi huku kukiwa na madai
kuwa majambazi hao hao, wanatumia sindano za sumu kuua watu.
Habari
kutoka kata za Kilema Kusini, Kilema Kaskazini na Marangu zinadai kuwa
mtandao wa majambazi hao wapatao 30, umekuwa ukilipiza kisasi kwa
wananchi wanaojitokeza kutoa ushahidi polisi. Wananchi hao wamependekeza
kutumika kwa sheria ya kuwaweka kizuizini watuhumiwa, ili kuepuka
uwezekano wa kuua watu.
Habari zilizozagaa katika Kijiji cha
Makami Juu, zilidai kuwa usiku wa Septemba 11 mwaka huu, majambazi
walimvamia mfanyabiashara, Respich Ngowi na kumuua kwa kumdunga sindano
ya sumu, “Waliiba kila kitu na wakamdunga sindano ya sumu, watu
hawakuthubutu kutoka nje ya nyumba wakihofia kukatwa mapanga na
kufuatiliwa na mtandao huo wa majambazi,”alidai mwananchi mmoja.
Wananchi
hao walidai kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na
madaktari, ulithibitisha kuwa mfanyabiashara huyo alichomwa sindano
mbili za sumu.
Mtandao huo ndio unaotuhumiwa kuilipua kwa
petroli, nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiraracha, Andrew Lekule na
kuteketeza mkewe na mtoto wao mdogo wa umri wa miaka mitano.
Mkazi
mwingine wa Kijiji cha Kitowo huko Kilema, alidai kuwa mtandao huo ni
kama umejitangazia “uhuru” kwa sababu unafanya uhalifu wakati wowote
wanapojisikia kufanya hivyo, “Ukiuza nguruwe wanakufuata usiku na hata
ukiuza mti wako wanakuja na mapanga wanataka pesa za mauzo. Hali si
nzuri hata kidogo karibu kata nzima ya Kilema Kaskazini,”alidai.
Hata
hivyo mkazi wa Kijiji cha Ruwa alilidokeza gazeti hili (MWANANCHI) kuwa
pamoja na jitihada za polisi kukamata washukiwa lakini wananchi
hawataki kutoa ushirikiano ikiwamo kuwatambua wahalifu, “Tatizo hapa ni
wananchi ambao hawana mwamko wa ulinzi shirikishi, yaani mtu anavamia
nyumbani na anapiga yowe la kuomba msaada, lakini hakuna jirani
anayetoka na kutoa msaada” alidai.
Mwananchi huyo ambaye naye
hakupenda jina lake litajwe, alidai kuwa kama wananchi wangekuwa na
umoja, wangeweza kusambaratisha mtandao huo.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kuwapo kwa matukio ya
ujambazi, lakini alisema tatizo ni wananchi wanaokataa kuwatambua
washukiwa wala kutoa ushahidi.
...soma zaidi habari hii ya Daniel Mjema katika gazeti la Mwananchi