Friday, September 21, 2012

AMUUA MKEWE MJAMZITO KWA KUMKATA NA SHOKA KICHWANI


Mkazi wa kitongoji cha Chang'ombee kijiji cha Kolang’a Kata ya Jaila, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga aliyefahamika kwa jina moja la Mvenelo (30), anadaiwa kumuua mkewe, Mwenjuma Digwele (25), kwa kumkata kichwa kwa shoka akiwa na ujauzito wa miezi minane.

Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Liwowa, lilitokea Septemba 17, mwaka huu saa 7:00 mchana katika kitongoji cha Chang’ombe.

Baadhi  ya watu waliofika muda baada ya tukio hilo, walidai kuwa walikuta kichwa cha mwanamke huyo kimetenganishwa vipande viwili, "Hata madaktari waliokwenda, walilazinmika kufanya kazi ya ziada kushona kichwa na kurudisha katika hali yake ya kawaida," alisema mmoja wa watu hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Hata hivyo, alisema sababu za mauaji hayo hawazifahamu lakini inahisiwa kuwa ni wivu wa mapenzi na mtuhumiwa alitoroka baada ya kutekeleza unyama huo.

Imedaiwa, kabla ya kufanya unayama huo, mume huyo aliwaamuru watoto wake kuondoka pale nyumbani waende kucheza.

Polisi wilayani Kilindi, wanalalamikiwa kwa madai ya kuushindwa kuchukua hatua mapema kutokana na kudokezwa mapema na Afisa Mtendaji wa Kata ya Jaila kuhusiana na kuwepo kwa mpango huo.

Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, alisema: "Polisi Kilindi wanastahili kubeba lawama, tukio lilitokea mchana lakini wao walifika siku iliyofuata, wana nia mbaya na Serikali ya CCM, malalamiko dhidi yao ni mengi.”

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Liwowa, alisema: "Tukio hili la mauaji linasikitisha mno, mtu kumuua mkewe tena mjamzito inasikitisha sana." via NIPASHE