Friday, September 21, 2012

MWANAFUNZI AJIFUNGUA AKIWA ANAMALIZA ELIMU YA MSINGI

Mwanafunzi wa darasa la saba amejifungua wakati akifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wilayani Muleba, Kagera.

Tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa nne na tano asubuhi katika Shule ya Msingi Kabiri katika Kijiji na Kata ya Kabirizi, Nshamba wakati mwanafunzi huyo, mwenye umri wa miaka 14 (jina na namba yake ya mtihani inahifadhiwa) akifanya mtihani wa pili na wenzake ndani ya chumba cha mtihani.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka shule hiyo, mwanafunzi huyo, alimwomba Msimamizi muda mfupi baada ya kuanza mtihani wa Hisabati, amruhusu kutoka nje kwa kuwa alikuwa akijisikia vibaya.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari kutoka eneo la tukio, baada ya mwanafunzi huyo kumwomba Msimamizi ruhusa, alimzuia akidhani ni ujanja wa kutaka kwenda kuchukua majibu, lakini baadaye aliona akijinyonganyonga.

“Msimamizi alimwuliza anaumwa nini akamwambia anaumwa tumbo na baada ya kuendelea kumhoji alimweleza wazi kwamba anaumwa uchungu, hali iliyomfanya Msimamizi aende kwa mmoja wa walimu wa shule hiyo na kumwomba msaada,” alisema mmoja wa watahiniwa hao na kuongeza: “Walimchukua na kumwingiza kwenye nyumba ya mwalimu huyo na kumfuata mkunga wa jadi ambaye alimsaidia kujifungua salama mtoto wa kiume”.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mtoto huyo alipewa jina la OMR, mfumo mpya maalumu unaotumika kujibu maswali ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, ambapo mwanafunzi anaainisha jibu sahihi kwa kusiliba kwa kalamu ya risasi.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya ya Muleba, Savera Celestine alithibitisha binti huyo kujifungua, lakini hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo, kwa madai kuwa mzungumzaji mkuu wa masuala yote ya mtihani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, “Ni kweli tukio hilo lipo, lakini mimi ndio nimefika hapa ofisini sasa hivi, sijapokea taarifa rasmi juu ya tukio hilo, lakini hata kama ningelikuwa nalo siwezi kulizungumzia kwa sababu anayepaswa kuzungumzia masuala yote ya mtihani huu ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, hebu mpigie atakupa taarifa,” alisema Kaimu Ofisa Elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mtihani ya Wilaya, Oliver Vavunge alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia tukio hilo, hakukiri wala kukanusha kuwapo tukio hilo na kusisitiza, kwamba atazungumza baada ya kupokea taarifa ya wilaya nzima kuhusu mtihani huo, “Kwa sasa niko huku kisiwani nashughulikia masuala ya mtihani, siwezi kuzungumzia jambo lolote la mtihani, natarajia kufanya hivyo kesho (leo) ambapo nitakuwa nimepata taarifa ya wilaya nzima, tena tutakuwa tumefanya majumuisho yote,” alisema Vavunge.

Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Ally Rajabu naye kwa njia ya simu, alikiri kutokea tukio hilo na kueleza kwamba baada ya mwanafunzi huyo kujifungua, alionekana kuchoka na walimtoa kwenye nyumba ya mwalimu na kumpeleka kwao.

Alisema hata hivyo, alikuwa chini ya ulinzi wa askari waliokuwa wakimsubiri apate nguvu ili ikiwezekana arejeshwe shuleni kuendelea na mtihani, ambao alipaswa kumalizia Hisabati na kisha kufanya mtihani mwingine wa Kiswahili ambao ulikuwa ukifuata.

Mkuu wa Wilaya, Lembris Kipuyo naye alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa kwa mujibu wa taarifa alizopewa na vyombo vya ulinzi na usalama kupitia Msimamizi wa Mtihani shuleni hapo, Christina Didas, mwanafunzi huyo aliendelea na mtihani wa Hisabati na baadaye wa Kiswahili ambao ulikuwa wa mwisho kwa juzi, “Ni kweli tumepatwa na tukio hilo na taarifa rasmi nilizonazo ni kwamba baada ya mwanafunzi huyo kujifungua salama, alipewa muda wa kupumzika na baadaye alirejea na kufanya mitihani yake yote na nimeelezwa kwamba leo (jana) pia kama hali yake itakuwa nzuri ataendelea na mitihani ya mwisho,” alisema Kipuyo jana alipozungumza na gazeti hili kwa simu.

Source:Habari leo