Friday, August 10, 2012

WANAKIBAMBA WAKIMBIA KWAO


Wakazi  wa Kibamba wilaya ya Kinondoni, jijini  Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo, wamezikimbia nyumba zao baada ya kutokea kishindo kikubwa cha milipuko katika Kambi ya Jeshi la Vifaru ilyoko Mloganzila,Kisarawe, Pwani.

Tukio hilo limetokea kati ya saa tano na 7:04 usiku ambapo milipuko hiyo ilikuwa mitano, ikiambatana na kukatika kwa umeme, mawasiliano ya simu pia kukiwa na mvua kubwa. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Fullshangweblog, wakazi hao walisema tukio hilo limewashtua kwasababu halijawahi kutokea katika miaka zaidi ya saba walioshi kwenye neo hilo.

Walisema waliamua kukimbia na kuelekea kusikojulikana kwa ajili ya kuokoa maisha yao.

Mmoja wa wakazi hao Mhando Yahaya alisema Wakazi wote wa Kibamba walikimbilia kwenye kijiji kidogo cha Kibwegele ambapo waliamua kuacha nyumba pamoja na mali zao bila kujali.
  
“Ujuwe serikali inabidi itowe angalizo kabla na siyo kufanya siri kwa kuwa matokeo ya siri ndiyo kama haya wananchi tunatishika na kukimbia hovyo usiku huu, mvua na giza vikituandama ”alisema Yahaya.

Naye Egnes Habiyu, alisema milipuko kama hiyo, imesababisha baadhi ya wagonjwa wa moyo kushtuka hadi kufikia hatua ya kuishiwa nguvu na kuanguka kwenye maji ya mvua ilyokuwa ikinyesha.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo, Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali, Kapambala Mgawe alisema hayo yalikuwa mazoezi ya kawaida na hayana uhusiano wowote wa kivita.

Vilevile aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa milipuko hiyo haina madhara bali ni moja ya mazoezi ya kawaida hivyo wawewatulivu.

Kanali, Mgawe alisema taarifa zilitolewa kwa wakazi wanaoishi jirani na kambi hiyo, bali kwakuwa yalifanyika usiku kukiwa kumetulia kumesababisha sauti ya milipuko hiyo kusikika mbali.