Monday, August 6, 2012

SERIKALI YAANDAA MPANGO WA ULIPAJI PENSHENI KWA WAZEE

Na Zawadi Msalla – Maelezo, Dodoma. 
 
SERIKALI inaandaa mpango madhubuti wa ulipaji pensheni kwa wazee kote nchini ili kuboresha maisha yao jambo ambalo litawafanya waishi maisha marefu zaidi.

Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa bungeni leo, Waziri wa
Kazi na Ajira Gaudencia  Kabaka alisema kuwa wizara yake imeandaa utaratibu utakaowasaidia wazee kulipwa pensheni kuanzia mwaka 2013.
Utoaji wa pensheni hiyo utaenda sambamba na uanzishwaji wa sheria mpya ya wazee inayotarajiwa kuanza kutumika mwaka 2013.

Awali akijibu swali la msingi Naibu Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii Dk. Seif Rashid alisema kuwa sheria  hiyo imejikita zaidi kutetea haki za wazee na kuboresha maisha  yao kwa
kuhakikisha kuwa wanatambuliwa na  kupewa fursa ya kushiriki kwenye mambo yanayohusu maisha yao
ya kila siku kwa manufaa ya watanzania wote.

“Wizara imekuwa ikishughulikia upatikanaji wa sheria hiyo,
rasimu ilishaandaliwa na kujadiliwa na wadau kwa hivi sasa  inafanyiwa maboresho ili
iwasilishwe katika ngazi ya sekretariet.” Alisema Dk. Seif.

Zoezi la kuandaa sheria hiyo linafanyika kwa awamu
ambapo Serikali itawasilisha Bungeni  mswada huo wa sheria mwezi Aprili mwaka  2013.

Hata hivyo kumekuwepo na malalamiko mbalimbali kwa
ucheleweshaji wa sheria hiyo ambayo kwa sasa  haki za msingi za wazee hazipewi kipaumbele zikiwezo za huduma za afya na maendeleo ya kila siku.

Akichangia mjadala huo Mbunge wa Viti Maalum  Magret Mkanga alishangazwa na ucheleweshwaji wa uanzishwaji wa sheria hiyo kwani
sera ya Taifa ya Wazee ilipitishwa mwaka 2003.

“Sera ya Taifa ya Wazee ilipitishwa mwaka 2003 hadi sasa miaka kumi imeshapita bado sheria haijaundwa, jambo hili linawafanya wazee
wapate huduma kwa huruma tu”, alisema.