Kutoka kwenye gazeti la MTANZANIA BAADA ya kufanyika kwa uchunguzi wa kitabibu kuhusu kifo cha mfuasi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Zona, matokeo ya
madaktari yamebaini jeraha lililosababisha kifo chake limetokana na
kugongwa na kitu kizito na si risasi kama ilivyokuwa inadaiwa.
Tukio
hilo lilitokea Agosti 27, mwaka huu mjini Morogoro, wakati polisi
wakitawanya maandamano ya wanachama wa chama hicho wakitokea eneo la
Msamvu Lupila kuelekea Viwanja vya Fire kulikofanyika mkutano huo ambapo
awali yalikatazwa na jeshi hilo.
Akieleza
matokeo ya uchunguzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile, alisema jeraha hilo la marehemu lililokuwa kichwani
lilitokana na kugongwa na kitu kizito kilichorushwa na si risasi kama
ambavyo watu walikuwa wakidhani.
Alisema
uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wawili wa mkoani hapa pamoja na
Dkt. Ahmed Makata kutoka Dar es Salaam na kushuhudiwa na mwanasheria wa
CHADEMA, Amani Mwaipaja, pamoja na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.
Alisema
baada ya matokeo hayo ya daktari, polisi sasa wanaendelea na uchunguzi
wa kubaini kitu hicho kilichorushwa na kusababisha kifo cha mfuasi huyo.
Alisema
baadaye watachukua hatua za kisheria kwa askari ama mtu mwingine
atakayebainika kuhusika kurusha kitu hicho, ikiwa ni pamoja na kumkamata
mtu ama kiongozi wa chama hicho aliyechochea ama kuandaa maandamano
hayo yaliyozua vurugu.
Alisema katika
kubaini mwenendo mzima wa tukio hilo, Serikali imeunda tume ya
kuchunguza ambayo inahusisha askari polisi na watu wengine watakaosaidia
kukamilisha uchunguzi huo.
Hata hivyo,
alisema tume hiyo ambayo tayari imeshafika mkoani hapa, itatafuta
maelezo na ushahidi kutoka kwa watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo,
wakiwamo wanahabari na kuwaomba wote watakaohitajika kutoa ushirikiano.
Akielezea
kuhusu majeruhi, Hashimu Seiph, aliyejeruhiwa mguu katika vurugu hizo,
alisema uchunguzi umebaini kuwa alijeruhiwa na bomu lililomuangukia
mguuni na anaendelea vizuri na bado yuko Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa
ajili ya matibabu zaidi.
Kwa upande
wake, Mwanasheria wa CHADEMA, Aman Mwaipaja, ulikiri kupokea taarifa ya
matokeo ya uchunguzi wa madaktari hao na kusema wanafanya mawasiliano na
viongozi wakuu wa chama hicho kuona hatua gani zitachukuliwa.
Alisema
kwa sasa anafanya mawasiliano na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad
Slaa, aweze kumpatia taarifa hiyo na hatua zozote zitakazochukuliwa
zitatolewa taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema
mwili wa marehemu huyo unatarajia kusafirishwa baada ya familia kukaa
na kupanga siku ya mazishi mkoani Tanga na mazishi hayo yatahudhuriwa na
baadhi ya viongozi wa CHADEMA mkoani Tanga na wengine.
