Taasisi ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha
Walimu Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili
kumaliza mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni
ni wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu
unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu
ambacho hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza
Serikali iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi
zao.
Mkurugenzi huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa
kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi wake haileti unafuu
wa maisha kwa watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya
kufanya kumaliza mgogoro huo.
“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu
endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi
ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu
na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu
walio hoi,” alisema Missokia.
Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku
wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani
wanamgogoro na Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
|