Mkazi wa
Ndembezi mjini Shinyanga amepigwa na mumewe hadi kuzirai na kukimbizwa
hospitalini kwa matibabu baada ya kutoa ushirikiano kwa karani wa Sensa ya Watu
na Makazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Evarist Mangala, alisema jana kuwa mwanamke
huyo, Esther Zablon (40) alipigwa juzi saa mbili asubuhi baada ya mumewe,
Ismail Yahya kupata taarifa kuwa karani wa sensa alifika nyumbani kwao na mkewe
kukubali kuhesabiwa na kutoa takwimu za familia yao.
Akisimulia, Kamanda Mangala alisema karani huyo alipokwenda nyumbani hapo, mume
hakuwapo na kama mkuu wa kaya, Esther akazungumza na kutoa taarifa.
Alisema baada ya mume kurudi nyumbani na kugundua kuwa mkewe alikubali
kuhesabiwa, alimshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha mke huyo kupoteza
fahamu.
Kutokana na kipigo hicho, kwa mujibu wa Kamanda Mangala, Esther alikimbizwa
katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi na matibabu.
“Wakati mwanamke huyo akichukua fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kituoni kabla
ya kufikishwa hospitalini, huku akilia kuwa sababu ya kipigo ni yeye kukubali
kuhesabiwa, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa dini ya mumewe (Uislamu),”
alisema Kamanda Mangala.
Hata hivyo, Kamanda alisema Esther alitoroka wodini kwa kuhofia mumewe kukamatwa
na hatimaye kufungwa.
Kamanda Mangala alisema Polisi wanaendelea kumtafuta Yahya na akipatikana
atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili. SOURCE WWW.WAVUTI.COM
