Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
SERIKALI inatarajia kuanzisha tuzo za umahiri kwa waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii (blogs) nchini kuanzia mwaka 2017.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Tanzania
Bloggers Network (TBN) na semina ya wanachama wa umoja wa waendeshaji wa
blog nchini.
Waziri
Nape alisema kuwa lengo la tuzo hizo ni kuzisaidia blogs za Tanzania
kubobea katika nyanja tofauti ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda, hifadhi
ya jamii kwa nia ya kuipa heshima tasnia ya habari nchini.
Aidha,
Waziri Nape alisema kuwa tayari Serikali imeanza mazungumzo
na makampuni na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo
ili kuhakikisha kuwa washindi wanapatikana kwa uwazi.
“Tuzo
hizo zitakuwa za kwanza kwa namna zitakavyoendeshwa kwa uwazi hivyo
makampuni zaidi yanakaribishwa kuweza kudhamini mashindano hayo
yatakayojielekeza kwenye nyanja tofauti” alisema Waziri Nape.
Waziri Nape pia alisema amewataka wamiliki na watendaji wa blogs nchini kushirikiana na Serikali ili kuweza kuijenga nchi.
“Tutumie
fursa za kisiasa zilizopo, fursa za teknolojia ili kuhakikisha
tiunajenga Tanzania tunayoitaka, ishaurini Serikali kwa kutumia taaluma
mliyonayo ili kuweza kuipeleka nchi ya Tanzania tunayoitaka” alifafanua
Waziri Nape.(P.T)
No comments:
Post a Comment