Friday, February 27, 2015

ZANZIBAR WAKIRI KUKAMATA KOBE 250 WALIOKUA WANASAFIRISHWA KWENDA MALAYSIA

Kobe wadogo 250, wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wakiwa njiani kusafirishwa kwa njia ya magendo kwenda Malaysia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, alisema kobe hao walikamatwa wakiwa wamehifadhiwa katika masanduku yaliyowekwa maembe ndani yake, katika hatua za mwisho za kusafirishwa.


“Ni kweli tumekamata kobe 250 wakiwa wamehifadhiwa vizuri katika masanduku yakiwa yameingizwa maembe tayari kusafirishwa kwenda Malaysia,” alisema.

Hata hivyo Kamanda Hamdani alikataa kumtaja mtu aliyekamatwa na kobe hao kwa madai kwamba uchunguzi unaendelea na kitendo cha kumtaja moja kwa moja, kinaweza kuharibu uchunguzi wa tukio hilo.

“Jeshi la Polisi kwa sasa halipo tayari kumtaja mtuhumiwa aliyekamatwa na kobe hao kwa sababu uchunguzi zaidi unaendelea...unajuwa ukianza kumtaja mtuhumiwa pamoja na watu wengine, unaharibu uchunguzi mzima wa tukio hilo,” alisema.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wizi wa kobe kutoka Zanzibar kupelekwa sehemu nyingine duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania Bara.

Kobe hao wanalindwa na sheria za kimataifa, wakiwa katika orodha ya viumbe ambao wapo katika hatari ya kutoweka duniani, kama ilivyo kwa kasa kwa hivyo wamekuwa katika udhibiti mkubwa.
Kwa upande wa Zanzibar, kobe wanahifadhiwa katika kisiwa kidogo cha Chumbe kilichopo nje ya Bandari ya Malindi umbali wa kilometa 40, ambapo hata hivyo kumekuwepo matukio ya wizi wa mara kwa mara.

Ofisa mmoja kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambaye moja ya majukumu yake ni kulinda na kuhifadhi kobe waliopo katika kisiwa kidogo cha Changuu, alikiri kuwepo wizi katika nyakati tofauti, unaofanywa na watu wasiokuwa waaminifu wanaotembelea kisiwa hicho kwa shughuli za utalii.

“Yapo matukio ya wizi wa kobe katika kisiwa cha Changuu kwa nyakati tofauti, kwani watu hufika katika kisiwa kwa shughuli tofauti ikiwemo za matembezi ya utalii,” alisema.

Katika miaka kumi iliyopita, zaidi ya kobe 1,500 wameibwa katika kisiwa cha Changuu, wakiwemo kobe wadogo ambao huhifadhiwa katika sehemu maalumu.

  • HabariLeo

No comments:

Post a Comment