Ukawa wakifafanua jambo
Wakati
CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea
wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa
Ukawa, Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo
mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani,
imefahamika.
Tangu
mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika nyingi za kisiasa ndani ya vyama
vya siasa na Jumanne iliyopita CCM ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini
Zanzibar na kutoa maazimio yanayogusia mchakato huo lakini ikasita
kutaja ratiba rasmi ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati
hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya
viongozi wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini Dar es Salaam Januari 20,
ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano wao, likiwamo suala la
kupata wagombea huku vikao vya ndani ya vyama vikitarajiwa mwishoni mwa
mwezi huu.(P.T)
Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho
Jumanne akisema kutakuwa na ajenda nyingine lakini: "Suala la kupata
wagombea nalo huenda likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa
Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda."
Ajenda
nyingine alizotaja ni mwongozo wa Ukawa, kura ya maoni ya Katiba,
changamoto za uandikishaji wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na
tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka
jana. Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema
watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta majibu ya changamoto
zilizopo kwa sasa.
Kiongozi
huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila chama ndani ya Ukawa kupitia
vikao vyake kitateua majina ya wagombea ambao watashindanishwa ndani ya
umoja huo, akisema kabla ya Machi, jina la mgombea urais ndani ya chama
chake litakuwa limeshapendekezwa.
Awali,
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema vikao vya chama
hicho vinavyotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na
ajenda ya uchaguzi vitakavyojadili mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda
yake inavyosema.
"Nadhani
vikao hivyo ndiyo vitaanza kujadili ajenda ya uchaguzi ujao. Tulishatoa
nafasi ya watu kujitokeza kwenye nafasi mbalimbali. Tukishapendekeza
majina ya wagombea kwa baadaye ndiyo tutawapeleka ili kuchambuliwa kwa
pamoja na kamati ya Ukawa.
"Mpaka
sasa kamati ya Ukawa inaendelea na kazi yake tangu Oktoba mwaka jana ila
inakuwa vigumu kwa wajumbe kujua kazi zote zinazofanywa na kamati hiyo
kutokana na msingi wa majukumu yake."
Nyambabe
alisema kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi, ikijumuisha wajumbe
wasiopungua watatu kutoka kila chama ili kufanya tathimini, kuchambua na
kuratibu shughuli zote za uchaguzi.
Kuhusu
kupata mwongozo wa Ukawa, Nyambabe alisema: "Namna ya kupata mgombea,
ilani moja na mwelekeo, vinaweza kuonekana kuanzia Februari baada ya
vyama kukaa vikao vyake."
Wakati
Nyambabe akisema hayo, kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari kuwa
CUF kimeshatangaza kumsimamisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwania urais,
ambazo hata hivyo, zimekanushwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara,
Magdalena Sakaya.
Alisema
kikao cha hivi karibuni ndani ya chama hicho kilikuwa na ajenda ya
kutathimini Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tu na hakukuwa na ajenda
nyingine iliyojadiliwa. "Bado hatujapendekeza jina lolote," alisema
Sakaya.
Hata
hivyo, Sakaya alisema kikao kijacho cha wenyeviti wa Ukawa hakitakuwa na
mamlaka yoyote ya kuamua au kupitisha jambo bila kupata baraka za
viongozi wa Baraza la Uongozi Taifa kutoka kila chama.
"Kikao
hicho sijafahamu ajenda yake lakini ifahamike tu kwamba, ndani ya Ukawa
kuna vikao vitatu; kikao cha maofisa, kikao cha makatibu na kikao cha
wenyeviti na hufanyika kwa kuzingatia ratiba zake," alisema na kuongeza:
"Kwa
hivyo utaratibu wa mgombea hauwezi kupatikana kwa sasa kwani hakuna
chama ambacho kimejadili ajenda yoyote au kupitisha majina ya wagombea
wake."
Sakaya
alisema kabla ya kujadiliwa ndani ya Ukawa, vikao vya mabaraza na kamati
kuu za vyama husika vitakuwa vimeshiriki kuchambua na kupitisha majina
ya wagombea wake wanaokidhi vigezo.
"Baada ya
hapo ndipo majina yatafikishwa Ukawa na kamati itachambua wanaoweza
kusimama kwa niaba ya Ukawa kutokana na tathimini yao watakayokuwa
wameipata," alisema na kuongeza:
"Kwa
upande wa CUF, kalenda yetu inaonyesha kuwa na vikao mwishoni mwa mwezi
huu. Nadhani kutakuwa na mwelekeo juu ya uchaguzi ujao." Viongozi wa juu
wa Chadema jana hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa
Habari wake, Tumaini Makene alisema kwa sasa chama hicho hakijafikiria
kuwa na vikao vyenye ajenda ya kuangalia jina litakalopitishwa kwa ajili
ya kuingia Ukawa...
"Bado
kabisa kuhusu suala la kujadili mgombea urais wa Ukawa, hatujafikiria
hilo ila kinachotuumiza akili kwa sasa ni kero za daftari la wapigakura
na kuwapo kwa tume isiyokuwa huru ya uchaguzi. Ratiba ya ajenda hiyo
ikitoka tutajulishana," alisema Makene.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment