Thursday, May 29, 2014

SUMATRA YAFUNGA KITUO CHA DALADALA MWENGE JIJINI DAR

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuhamisha kituo maarufu cha daladala cha Mwenge kwenda eneo la Makumbusho.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, ofisa mfawidhi wa Sumatra wa Kanda ya Mashariki, Conrad Shio alisema Kituo cha Mwenge kitafungwa rasmi Jumapili na eneo hilo litabaki wazi kupisha upanuzi wa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Shio alieleza sababu ya kuhamisha kituo hicho kuwa ni ufinyu wa eneo lenyewe jambo linalosababisha magari kushindwa kuingia kituoni hapo kwa wakati, hasa nyakati za asubuhi na jioni. Hali hiyo husababisha foleni kubwa isiyo ya lazima.

Alisisitiza madereva wote kutii agizo hilo kuanzia Jumatatu na kwamba atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria. Pia, aliwataka abiria kutolazimisha kushushwa katika eneo hilo wakati hakuna kituo. Shio aliongeza kuwa barabara za kuingia na kutoka Kituo cha Makumbusho bado zinakarabatiwa na Manispaa ya Kinondoni ili kurahisisha uingiaji na utokaji wa magari katika kituo hicho.

Hivi karibuni, madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Mwenge, Tegeta na Ubungo waligoma kutoa huduma kushinikiza Serikali kueleza kituo mbadala baada ya kufungwa kwa kituo cha Ubungo kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.

No comments:

Post a Comment