Wednesday, April 16, 2014

MTIKILA "WAKATI WA KUDANGANYANA KUHUSU MUUNGANO SASA UMEKWISHA


Mjumbe  wa Bunge Maalum la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema kuwa hivi sasa ndiyo muda mwafaka wa Watanzania kuambiana ukweli kuhusu Muungano. Mchungaji Mtikila (pichani) alitoa kauli hiyo bungeni jana alipoomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sitta, baada ya mjumbe Tundu Lissu, kutoa ufafanuzi wa wa maoni ya wajumbe wachache wa Kamati namba 4.

Mchungaji Mtikila baada ya kuruhusiwa kuzungumza, alisema alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 50 Watanzania hawajawahi kuambiwa ukweli kuhusu Muungano na kusema kwamba badala yake wamekuwa wakiambiwa uongo na kwamba ndiyo maana Mungu hakuibariki Tanzania kwa kipindi hicho chote.

“Tulijengwa katika uongo na ndiyo maana Mungu hakutubariki kwa miaka 50,” alisema Mchungaji Mtikila.

Mchungaji Mtikila akijibu kauli ya Peter Serukamba, aliyehoji kuwa wajumbe hao wapo bungeni hapo kama nani kama Muungano hauna uhalali kama alivyosema Lissu, alisema:

Ndiyo maana tumekuja kufanya kazi ya kutengeneza Katiba na kuandika upya historia.”

Mchungaji Mtikila alisema kwamba hivi sasa Tanzania ina watu milioni 45 na kwamba hakuna sababu ya kuendelea kuwaeleza uongo kuhusu historia ya Muungano.

Mchungaji Mtikila ambaye kwa miaka mingi amekuwa akiupinga Muungano, alisema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuambiana ukweli.

Aliongeza kuwa Watanganyika wanahitaji kuwa na haki ya kupata serikali yao pamoja na Wazanzibari kujitambua na kuwa na taifa lao.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment