Friday, February 14, 2014

MAITI YAPIGWA MAKOFI,PIA YASUSWA NA NDUGU ZAKE HOSPITALI WAZIKA NI YA YULE JAMBAZI ALIYEUA WATU 9 MUSOMA

 


MAZIKO ya mtuhumiwa wa mauaji ya watu tisa na unyang'anyi wilayani hapa, Charles Kichune, yamesuswa na ndugu zake. Tangu Kichune afariki dunia Februari 9 kwa ugonjwa wa pumu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, hakuna ndugu aliyefika kuchukua mwili huo.
Kutokana na kukaa mochari kwa muda mrefu na kuharibika, Halmashauri ya Mji ililazimika kusitiri mwili huo kwa kuuzika jana.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Tarime, Dk Michael Nega alisema walilazimika kumzika baada ya kukaa muda mrefu bila ndugu zake kujitokeza.
“Imetulazimu kwenda kumzika Kichune kutokana na ndugu zake kuususia mwili mochari ya hospitali hii na kuharibika na kutoa harufu kali,” alisema Dk Nega.
 
Katika hali isiyo ya kawaida Jumapili iliyopita baada ya kufariki dunia kwa Kichune, mmoja wa wakazi wa Tarime aliyefika kutambua mwili huo, alilia na kuupiga makofi. Mkazi huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja, inadaiwa amefiwa na wajukuu zake wawili, David Yomami na Samwel Richard, ambao wanadaiwa kuuawa na Kichune.
Vijana hao wawili waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wakitengeneza gari lao lililokuwa limeharibika. Kichune alikuwa na majina zaidi ya moja ambapo katika baadhi ya maeneo alikuwa akitambulika kama Josephat Chacha au Charles Msongo.
Polisi inadai baada ya kukamatwa, alikiri kuhusika na mauaji ya watu mbalimbali katika kata za Binagi, Turwa na Kitare katika vijiji vya Mogabiri, Kenyamanyori, Nkende na Rebu.
Kichune alikamatwa Februari 6 Tanga alikokuwa akifuatiliwa na Polisi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Baada ya kukamatwa, uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa baada ya mauaji ya watu tisa, alikodi pikipiki kutoka kijiji cha Kenyamanyori alikokuwa akiishi, hadi Musoma.
Alipofika Musoma, inadaiwa alihifadhi bunduki aina ya SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake, Marwa Keryoba maeneo ya Bweri na alipokamatwa alimtaja Keryoba kuwa ndiye anayetunza silaha hiyo. Februari 7, Polisi walifuatilia silaha hiyo kwa Marwa na kumkuta mtuhumiwa, ambaye alitakiwa kujisalimisha lakini alikaidi na kuwarushia risasi askari.
“Marwa aliuawa Februari 7 alfajiri maeneo ya Bweri mjini Musoma, alipotakiwa kujisalimisha na kukaidi na kuanza kurushiana risasi na askari," alisema Kamanda Kamugisha.CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment