Tuesday, December 17, 2013

LIYUMBA: "SIKUWA NA SIMU GEREZANI" SOMA ZAIDI HAPA....

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba amekana kukutwa na simu gerezani na kudai amebambikiwa kesi hiyo ili aendelee kukaa gerezani.
Liyumba anakabiliwa na kesi ya kukutwa na simu wakati alipokuwa gerezani, kutumikia kifungo chake cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.
Hata hivyo, Liyumba ambaye alijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi alipofunga ushahidi wake. Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Augustina Mmbando alipanga kutoa hukumu Januari 15, mwakani.

Awali akiongozwa na Wakili, Hudson Ndusyepo, Liyumba alidai kuwa mipango ya kumbambikizia kesi ilianza miezi miwili kabla hajamaliza kutumikia kifungo chake na uliwahusisha askari magereza saba. 

Alidai kuwa, mchana wa Julai 27, mwaka juzi, akiwa na mahabusu anayejulikana kwa jina la Mkenya wakisoma magazeti katika chumba chake cha selo, waliingia askari wawili na kumwambia awaeleze alipoipata simu ambayo ilikuwa imeshikwa na mmoja wa askari hao aitwaye Patrick. 

“Nilipoulizwa swali hilo nilishituka na kupata shinikizo la damu, nikawauliza kwanini mnanionea, nimechoka kuonewa?” alidai Liyumba. 

Alidai askari hao walimchukua na kumpeleka Ofisi ya Mkuu wa Usalama wa Gereza, ambako aliwakuta askari watano waliokuwa wanamsubiri na kuanza kumshambulia kwa maneno kuwa anaringa. 

Liyumba, ambaye alitumikia BoT kwa miaka 35, alidai simu hiyo aliingia nayo Patrick ambaye alikuwa shahidi wa upande wa mashitaka kwa sababu gerezani kulikuwa na ulinzi hivyo hakuna mfungwa wala mahabusu angeweza kuingiza simu. 

Akielezea mfululizo wa matukio anayodai yalipangwa Liyumba alidai, awali alishitakiwa kwa kuisababishia serikali ya hasara Sh bilioni 261 na baadaye hati ilibadilishwa akadaiwa kutumia madaraka vibaya wakati hakuwa nayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. 

Aliendela kudai kuwa wakati akiwa gerezani miezi miwili kabla ya kumaliza kifungo chake, Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walimfuata na kutaka kumbambikia kesi, alipotaka kuwa na wakili wake wakaachana naye, na sasa katuhumiwa kukutwa na simu gerezani. 

Alidai simu hiyo aliyodaiwa kukutwa nayo yenye namba 0653004662, haifahamu na upande wa Jamhuri umeshindwa kumleta mtaalamu mwenye orodha ya matumizi yake ili kujua mawasiliano yake na kama angepatikana na simu angepewa adhabu ya Mkuu wa Gereza. 

Alidai kama kweli walimkuta nayo, kwanini hawakumkamata na Mkenya au angekuwa shahidi na kuongeza kuwa mashahidi walitoa ushahidi dhidi yake walikuwa wamepandikizwa kwa lengo la kumuumiza ili aendelee kukaa gerezani na kuomba mahakama ifute mashitaka dhidi yake. 

Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, mwakani atakapotoa hukumu na kuzitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisha ya hoja Desemba 30, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment