Sunday, December 15, 2013

HIVI NDIVYO HALI ILIVYO BAADA YA MWILI WA MAREHEMU MANDELA

 

Qunu. Huzuni na simanzi viliyateka maeneo ya Mthatha na Qunu katika Jimbo la Eastern Cape, Afrika Kusini baada ya kuwasili kwa mwili wa rais wa kwanza mzalendo wa nchi, Nelson Mandela.

Mwili wa Mandela uliwasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha saa 7:40 mchana (kwa saa za huku) dakika 20 kabla ya muda uliotarajiwa, ukiwa umesafirishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria.

Ulisindikizwa na maofisa waandamizi wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), maofisa kutoka Serikali, wawakilishi wa familia yake na viongozi wa mila kutoka kabila la abaThembu.

Mandela anazikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Qunu ambako alikulia, katika mazishi ambayo yatakuwa mchanganyiko wa mila na desturi, dini yake ya Kikristo ikifuata taratibu za kimethodisti na kijeshi kwa maana ya Serikali,

 Alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo, Julai 18, 1918 na alifariki dunia Desemba 5, mwaka huu nyumbani kwake, Houghton, Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuugua magonjwa ya figo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Maziko yake yanamaanisha kuhitimishwa kwa siku 10 za maombolezo ya kitaifa, ambayo yalishuhudia mamia ya viongozi kutoka pande zote za dunia, waliofika Afrika Kusini kushiriki Ibada ya Kitaifa iliyofanyika katika Uwanja wa FNB, Soweto   Jumanne iliyopita.

Kadhalika mwili wa kiongozi huyo kwa siku tatu mfululizo; Jumatano hadi Ijumaa wiki hii ulikuwa ukiwekwa katika Ikulu ya Pretoria iliyopo Majengo ya Umoja (Union Buildings) ambako waombolezaji zaidi ya 100,000 walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.

Serikali ya Afrika Kusini imetaganza kuwa leo ni siku ya mapumziko huku wamiliki wa maduka makubwa nao wakitangaza kwamba hawatafungua biashara zao kama hatua ya kuienzi siku ya mwisho ya Mandela.

 Rais Jakaya  Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce Banda ni wakuu wa nchi pekee ambao watahudhuria mazishi ya Mandela na wote wamepangiwa kutoa salaamu za rambirambi wakati wa mazishi. Watawaongoza viongozi wengine kadhaa wakiwamo wale wanaowakilisha mashirika ya kimataifa.

Simanzi uwanjani

Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulikuwa kimya hasa baada ya ndugu wa karibu wa Mandela, wakiongoza na mjane Graca Machel kuwasili saa 6:44 mchana na kulakiwa na viogozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa Nqakula.

Mara baada ya jeneza kushushwa kutoka kwenye ndege ya jeshi Namba C-130, wimbo wa taifa ulipigwa, pia kupokea heshima kutoka kwa askari wa SANDF ambao walikuwa uwanjani hapo mapema.

No comments:

Post a Comment