Friday, June 7, 2013

MTIZAME MCHEZAJI WA WA MOROCCO AMBAYE KOCHA WA TAIFA STAR AMEKIRI KUMUOGOPA


Ni wa kuchunga; Kocha Kim akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Pullman mjini hapa kuhusu Belhanda. Kulia ni Nahodha Juma Kaseja.
Na Mahmoud Zubeiry, Marakech, IMEWEKWA JUNI 7, 2013 SAA 6:00 MCHANA KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba, kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji Morocco kuwania tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia, anamuhofia sana mshambuliaji wa Simba hao wa Atlasi, Younes Belhanda (23) wa Montpellier ya Ufaransa. 
Wa kuchunga; Belhanda, mchezaji tishio wa Morocco
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo asubuhi katika hoteli ya Pullman, Marakech, Poulsen alisema mchezaji huyo ana kila sababu ya kucheza vizuri kesho ili kuzidhihirishia klabu za Ulaya zinazotaka kumng’oa Montpellier kwamba yeye ni bora.  “Anatakiwa na Inter Milan, AC Milan, Galatasaray na Aston Villa na dau lake ni Pauni Milioni 20 na klabu yake tayari imekubali kumuuza. Hivyo huyu ni kati ya watu ambao wananifanya niifikirie mechi ya kesho itakuwa ngumu,”alisema. Pamoja na hayo, Poulsen alisema kwamba vijana wake wapo vizuri na wanampa matumaini makubwa kuelekea mchezo huo, ambao amepanga kucheza kwa mfumo wa kushambulia zaidi. 
Wazee wa NSSF; Magori na bosi wake Dk. Dau


Hans Poppe kulia na Michael Mukunza wa Executive Solutions, Waratibu wa udhamini wa Kilimanjaro Lager kwa Taifa Stars

Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager leo jioni itacheza kwenye Uwanja wa Marakech ili kuuzoea kabla ya  mtangange huo wa kesho, ambao utaanza Saa 3:00 usiku za hapa, sawa na saa 5:00 usiku za nyumbani Tanzania.
Kim amesema lengo ni kushinda kesho ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Belhanda anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na winga ni hatari kweli na kocha wake wa sasa, Rene Girard anamfananisha na mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Robert Pires aliyewika Arsenal.
Hadi sasa, Kim amekwishaiongoza Stars katika mechi 11, tangu arithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen Mei mwaka jana akipandishwa kutoka timu za vijana. 
Katika mechi hizo, Kim ameiwezesha Stars kushinda mechi tano, sare nne na kufungwa mbili tu, akiweka rekodi ya kushinda nyumbani mechi tano mfululizo, kati ya hizo mbili za mashindano. 
Juni 10, mwaka jana aliifunga 2-1 Gambia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya Kundi C kufuzu Kombe la Dunia, kabla ya Novemba 14, mwaka huo kuilaza Kenya, Harambee Stars 1-0, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza bao pekee la beki Aggrey Morris Ambroce na Desemba 22, mwaka huo pia aliwalaza waliokuwa mabingwa wa Afrika, Zambia 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la kiungo mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa, zote zikiwa mechi za kirafiki. 
BIN ZUBEIRY na Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe

Februari 6, mwaka huu alicheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu nyumbani na kuibuka na ushindi wa 1-0, dhidi ya mabingwa wa zamani wa Olimpiki, Cameroon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la Mbwana Samatta.
Machi 24, mwaka huu katika mchezo wa kwanza na Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, aliilaza 3-1 Morocco, mabao ya Samatta mawili na Thomas Ulimwengu moja.
Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Stars ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya bila mabao.
Kabla ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa hotuba nzuri. 
Mkuu wa Msafara wa Stars, Cresscentius John Magori yupo hapa kikamilifu na baadhi ya wadau wa soka, akiwemo Mbunge Zitto Zuberi Kabwe, Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Ushindi, Dk Ramadhan Dau, mfanyabiashara Zacharia Hans Poppe na wengineo na amesema; “Mambo yanakwenda vizuri”. 
Credit to Bin zubery

No comments:

Post a Comment