Kesi FIFA; Malipo ya manunuzi ya Emmanuel Okwi limefika FIFA |
Na Mahmoud Zubeiry SIMBA SC imetuma malalamiko Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, kuchelewa kulipa fedha za manunuzi ya mchezaji Mganda Emanuel Okwi, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 450 za Tanzania. Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Simba SC zimesema kwamba, Wekundu hao wa Msimbazi wametuma malalamiko hayo kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).“Tunasubiri majibu, tumetuma malalamiko hayo kwa mujibu wa taratibu kupitia TFF, imekuwa muda mrefu sasa tangu tufanye biashara hii Januari (mwaka huu),”kilisema chanzo kutoka Simba SC. BIN ZUBEIRY iliwasiliana na Ofisa wa TFF anayeshughulikia suala hilo, Saad Kawemba ambaye alisema kwamba bado lipo kizani. Kawemba alisema kwamba kwa mujibu wa taratibu za usajili kimataifa, Sahel wana nafasi ya kuilipa Simba SC fedha hizo ndani ya miaka miwili ya mkataba waliyoingia na Okwi. “Wanatakiwa walipe kabla hawajamaliza mkataba na Okwi, wanaweza kufanya hivyo, ila wakiwa waungwana watalipa mapema. Na hawawezi kuvunja mkataba na mchezaji kabla ya kulipa,”alisema Kawemba. Habari zaidi zinasema, Sahel imeingiwa kigugumizi cha kulipa fedha hizo Simba SC baada ya kuanza kukerwa na tabia ya Okwi kuchelewa kujiunga na timu kila anaporejea kwao kuchezea timu ya taifa. “Okwi anachangia sana sisi kucheleweshewa hizi fedha, maana ameanza mapema zile tabia zake alizokuwa anafanya hapa Simba, akienda kwao kuchezea timu ya taifa anachelewa kurudi, na kule anafanya hivyo hivyo. Sasa ile klabu imetupigia sisi kulalamikia tabia za Okwi kutoheshimu wajibu wake na inajuta kumnunua. Kwa kweli tabia hii Okwi lazima aachane nayo haraka sana, vinginevyo hawezi kucheza popote,”kilisema chanzo kutoka Simba SC.
No comments:
Post a Comment