Wednesday, March 20, 2013

WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI FOREST MBEYA WAANDAMANA KUTOKUWA NA IMANI NA MKUU WAO WA SHULE


Wanausalama wakifika katika shule ya sekondari Forest kutuliza maandamano yao

Wanafunzi sasa wametulia kumsikiliza Afisaelimu mkoa wa Mbeya aliyefika shuleni hapo kusikiliza kero zao
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda akiwasisitizia wanafunzi hao kuwa waache tabia ya kuandamana wajuwe kuwa wamekuja kusoma siyo kuandamana
Moja ya wanafunzi akimweleza kero yao afisa elimu mkoa Mbeya
Mkuu wa Shule  Cesilia Kakera akiwa amejishika kichwa baada ya wanafunzi kutokuwa naimaninae kwa kushirikiana na walimu wanaotuhumiwa kupokea rushwa shuleni hapo
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amesema suala la walimu hao kukamatwa na kufikishwa Takukuru ni suala la ngazi nyingine hivyo hawatakiwi kulizungumzia. 

Hii ndiyo ofisi inayotumika kuwatesa wanafunzi ofisi hii huitwa guantanamo bay camp
IKIWA zimepita siku chache tangu Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya kuwakamata Walimu wawili wa Shule ya Sekondari ya Forest wakituhumiwa kupokea rushwa sakata hilo limechukua sura mpya baada ya wanafunzi wa shule hiyo kuandamana.

Maandamano ya wanafunzi hao yametokana na Walimu hao kuwa nje ya dhamana na kuendelea kufundisha katika shule hiyo jambo ambalo wanafunzi hao wamelipinga na kusababisha maandamano yaliyozuiliwa na jeshi la polisi walipokuwa wakitaka kuelekea kwenye Ofisi za Ofisa Elimu wa Mkoa.

Kutokana na hali hiyo Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amelazimika kufika Shuleni hapo kisha kuzungumza na wanafunzi ambao walimtajia sababu zaidi ya kumi zilizosababisha kufanya maandamano hayo.
  
Wamezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na sakata la walimu waliokamatwa kwa rushwa kuachiwa na kuendelea kufundisha, Walimu kutofundisha, Vitisho vya walimu kwa wanafunzi, Wazazi kutukanwa na walimu, Kutokuwa na imani na Mkuu wa Shule pamoja na ujirani wa walimu watuhumiwa na mkuu wa Shule.

Wamezitaja sababu zingine kuwa ni Mkuu wa shule kutumia matofali ya shule kujengea madarasa badala ya wigo,kutokuwa na vifaa vya michezo pamoja na kutotolewa kwa vibali vya kwenda kucheza na shule jirani.

Wameongeza kuwa Shule haifanyi mikutano ya wanafunzi( baraza la shule la wanafunzi), kutokuwa na vitambulisho vya wanafunzi, michango ya wigo, michango ya wigo wa shule na michango ya masomo ya jioni.
  
Akijibu tuhuma hizo Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amesema suala la walimu hao kukamatwa na kufikishwa Takukuru ni suala la ngazi nyingine hivyo hawatakiwi kulizungumzia.
  
Kuhusu madai ya walimu kutofundisha Kaponda amesema si sababu ya kweli kutokana na wanafunzi hao kuwa kwenye mitihani ya kufungia mhura hivyo walimu hawawezi kuingia madarasani kufundisha.
  
Pia amewaagiza walimu hao kuwa na ushirikiano na wanafunzi na kutotoa lugha za vitisho kwa wanafunzi ambapo pia aliwaagiza wanafunzi kuwa watulivu na kuwasikiliza walimu wao.
  
Aidha amewaagiza walimu haokutoitisha mikutano ya wazazi pasipo kuwepo kwa bodi ya shule ambapo ameagiza kuwa kila mkutano wa wazazi utaklapofanyika ni vema mwenyekitiwa bodi ( ya shule akaongoza mikutano hiyo.
  
Kuhusu suala la vibali vya michezo, mikutano ya baraza la wanafunzi na vitambulisho Ofisa huyo aliagiza Mkuu wa Shule  hiyo Cesilia Kakera kulishughulikia mara moja na kumpelekea taarifa ofisini kwake mara moja.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka alipoulizwa suala la walimu hao kuendelea na kazi ili hali walikuwa wamekamatwa kwa tuhuma za rushwa Kamanda huyo alisema wameachiwa kwa dhamana.
  
Mtuka amesema baada ya watuhumiwa hao ambao walikamatwa Machi 4, Mwaka huu bado wanashikiliwa na kikosi chake ingawa wako nje kwa dhamana na kuongeza kuwa uchunguzi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo hawawezi kuwazuia kuendelea na kazi.
  
Amesema baada ya kukamilika uchunguzi ndipo itakapojulikana ni hatua ipi itakayofaa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa kama watakuwa wamebainika kuhusika na sakata hilo.

Walimu hao walikamatwa kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya kati ya shilingi 500 na 1,000 kutoka kwa wanafunzi wanaochelewa kufika shuleni asubuhi kila siku.
  
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka, alisema walimu hao walikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo baada ya kuchoshwa na tabia hiyo.
  
Mtuka amewataja walimu hao kuwa ni Solomoni Mwasote na Faustin Robert ambao walikamatwa shuleni hapo wakiwa wanaendelea na zoezi hilo la kuwalipisha wanafunzi fedha.

No comments:

Post a Comment