Wednesday, March 20, 2013

Injini za kisasa zinahitajika ili kuboresha usafiri wa Reli nchini

Dk. Harrison Mwakyembe
Na Hussein Makame na Genofeva Matemu-Maelezo

WAZIRI wa Uchukuzi,  Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali inahitaji injini za kisasa ili kuboresha usafiri wa treni kwa mkoa wa Dar es Salaam na reli ya kati kwa ujumla.

Dk. Mwakyembe  ameyasema  hayo leo (jana) wakati akiongea na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu walipotembelea mradi wa reli wa kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam .

Alisema kuwa iwapo injini hizo zitapatikana zitaipunguzia Serikali gharama kubwa kwa kuwa zinatumia mafuta machache na zinakwenda kwa kasi na kutoa faida mara tatu ya inayopatikana sasa kwani zinatumia  vichwa viwili vya treni na mabehewa nane kwa usafiri wa Dar es Salaam.

“Gharama za injini hizi ni Dola za Kimarekani milioni 6 ambazo Serikali imeshindwa kuzipata  kutokana na uwezo mdogo wa kifedha iliyonayo .Hivyo basi juhudi za pamoja zinahitaji baina yetu sote  ili kuiboresha sekta hii ambayo ni mhimili wa ukuaji wa uchumi wa nchi” , alisema Dk. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Peter Serukamba aliishauri serikali ijitahidi kuboresha mradi wa reli wa kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam ili kuongeza faida inayopatikana katika huduma hiyo.

Naye msemaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Midladjy Maez alisema kuwa gharama za uendeshaji wa mradi huo ni kubwa, hivyo basi alipendekeza kuboreshwa na kuimarishwa kwa njia za treni na kumalizia ujenzi wa vituo vya stesheni za njiani.

Maez alisema, “Kwa wakati huu TRL haiwezi kumudu gharama za uendeshaji wa treni hii, kwa hiyo tunaiomba Serikali itoe ruzuku ili TRL iweze kupunguza hasara inayoipata kila mwezi.

Wajumbe wa kamati hiyo walifanya ziara ya siku moja ya kutembelea mradi huo ili kuona maendeleo yake na changamoto zilizoko na kuona ni jinsi gani wanaweza kuzitatua ili  kuboresha huduma ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia reli.

No comments:

Post a Comment