Thursday, March 21, 2013

TANGAZO LA CONDOM LAONDOLEWA BAADA YA WANANCHI NA VIONGOZI WA DINI KULALAMIKA

Nairobi,Kenya Tangazo moja linalowaonesha akina mama wawili wakiwa gulioni limeondolewa kwenye vituo vya televisheni nchini Kenya baada ya kulalamikiwa na viongozi wa dini.

Katika tangazo hilo (ambalo limepachikwa hapo chini) mwanamke mmoja anamwuliza mwenziye kuhusu mahusiano yake na mumewe na kujibiwa kuwa mume amekuwa mlevi siku za hivi karibuni na anashinda kilabuni.

Tangazo linaendelea ambapo mwulizaji anauliza kuhusu “mpango wa kando” (hawara) ambapo anayeulizwa anamkodolea macho hawara yake aliye katika meza nyingine akiendelea na biashara ya kuuza matunda, huku akisema “anaridhishwa” naye, hata ikiwa hapati muda mwingi wa kuwa naye.

Ndipo mwuliza swali anauliza endapo wawili hao wanatumia condom, ambapo kwa aibu, anayeulizwa anazubaa kimya.

Karibu na mwisho wa tangazo hilo anasikika shoga akimshauri mwenziye juu ya umuhimu wa kutumia condom ili kujilinda yeye na wale anaowapenda, na kuisha kwa binti anayeonekana kuvalia sare ya shule, akimkimbilia mama na kumkumbatia, kisha linatamatia kwa maneno, “Weka Condom Mpangoni”.

Viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam wamesema sababu ya kulipinga tangazo hilo ni kwa kuwa linachochea “mpango wa kando” (usaliti katika ndoa na mahusiano), uzinzi na gono kabla ya umri (uasherati) badala ya kusisitiza juu ya ngono salama ili kukabiliana na maambuki za VVU/UKIMWI.

Wakailaumu tume ya mawasiliano nchini humo (CCK) kwa kushindwa kulichuja tangazo hilo.

No comments:

Post a Comment