Monday, March 25, 2013

NYOTA WA SIMBA STARS WAPAA LEO KWENDA KUONGEZA NGUVU BUKOBA

Juma Kaseja kulia na Amri Kiemba; Njiani kuelekea Bukoba

Na Mahmoud Zubeiry WACHEZAJI watano kati ya sita wa Simba SC waliokuwa katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichocheza na Morocco jana, wameondoka leo asubuhi Dar es Salaam kwenda Bukoba kuungana na wenzao tayari kwa mchezo wa keshokutwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Kagera Sugar. Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wachezaji walioondoka na ndege leo ni kipa Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe na viungo Amri Kiemba na Mrisho Ngassa. Kamwaga, ukipenda muite Mr. Liverpool alisema mchezaji aliyeachwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto ambaye hayumo katika mipango ya kocha Mfaransa, Patrick Liewig kwa sasa. “Hivi ninavyozungumza na wewe nipo na hao wachezaji Mwanza, tunasubiri kuunganisha ndege kwenda Bukoba leo leo,”alisema Kamwaga. Tayari wachezaji wa Simba SC ambao hawakuwamo Taifa Stars, wapo Bukoba tangu jana kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu. Mwandishi huyo wa zamani wa magazeti ya Dimba, Bingwa, Mtanzania, Rai na The African, yanayochapishwa na kampuni ya New Habari, alisema wachezaji hao wako fiti kabisa kwenda kuitumikia Simba SC. Aidha, Kamwaga alisema wachezaji wengine wawili waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes kilichomenyana na Liberia jana, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde nao wataungana na timu moja kwa moja Bukoba. “Mudde na Dhaira watakuja moja kwa moja Bukoba, kwa kweli wakipatikana wachezaji wote hawa hadi kesho asubuhi, kikosi kitakuwa imara sana na matumaini ya kuwafunga Kagera Sugar kwao yatakuwa makubwa,”alisema. Simba ambayo ni kama imekwishavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, kutokana na kuzidiwa pointi 14 na wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza kwa pointi zao 48, inapigana kuhakikisha japo inakuwa ya pili kwa kuipiku Azam iliyo katika nafasi hiyo kwa pointi zake 37. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 34.
 Habari kwa hisani ya Bin Zuberi

No comments:

Post a Comment