Tuesday, March 5, 2013

MBATIA AMTAKA WAZIRI MKUU KUWEKA WAJUMBE WATANO WAALIMU KATIKA TUME YA KUCHUNGUZA CHANZO CHA KUSHUKA KWA UFAULU WA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE,,, Haya ni miongoni mwa yaliyomo katika Barua aliyomuandikia Waziri Mkuu.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Mh, James Mbatia, amemtaka Waziri Mkuu Kubadilisha Tume aliyoiunda siku za karibuni ya kuchunguza tatizo la kufeli kwa watahiniwa wa Kidato cha nne kwa mwaka 2012 na  kumshauri kuwaweka wajumbe angalau 5 ambao ni walimu walioko kazini kwa sasa.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Ofisi hiyo yaliyopo jijini Dar es Salaam.

Mh, Mbatia amesema kuwa Waziri Mkuu kufanya hivyo ataifanya Tume iweze kuwa na Ufanisi endelevu kwani Uchungu wa Mwana aujuaye ni Mzazi, na mzazi hapa ni Mwalimu.

Amesema kuwa, kama kuna ulazima wa Serikali kuunda Tume jambo la kuzingatia ni hilo tajwa hapo juu ikiwa ni pamoja na Tume itakayoundwa kufanya ulinganifu wa Uzito wa Sababu zote zilizopo ya kuwa ni ipi nzito zaidi kwa kufuata viwango vya Kitaifa, kimataifa na uwezo tulionao kirasilimali.

Ameendelea kusema kuwa, ni vyema maafisa wa Serikali kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu kusoma taarifa mbalimbali za tafiti juu ya Swala zima la  kuporomoka kwa Elimu mathalani zilizoko katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Haki Elimu, Twaweza nk.

Amezungumzia pia swala la yeye kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume iliyoundwa na waziri Mkuu na kusema kuwa hajapata taarifa rasmi kwa maandishi kutoka katika ofisi ya Waziri mkuu na kusema kuwa kama ameteuliwa hajajua ni vigezo gani vilivyotumika kumuweka yeye kuwa mjumbe wa Tume hiyo.

Aidha amesema kuwa katika mkutano wa Bunge wa 10 (January/February 2013)b aliwasilisha hoja Binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya Elimu nchini ambapo alitoa maelezo juu ya Udhaifu wa Chimbuko hilo.

No comments:

Post a Comment