MTU mmoja anayesadikiwa kuwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya,
amekamatwa na Polisi mkoani Kilimanjaro katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na kilo 6 za unga wa Cocaine.
Mtu
huyo aliyefahamika kwa jina la Iddi Hassan Chumu (34), alikamatwa
uwanjani hapo Februari 2, majira ya saa 3:45 jioni, akiwa anataka
kusafiri kuelekea Hungary kwa kutumia ndege ya Qatar Airways kupitia
Doha.
Taarifa hizo zinasema kuwa Chumu alikuwa ameficha unga huo ambao kwa sasa umepelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya vipimo zaidi.
Chumu
anadaiwa ni mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, ambapo kwa sasa
anashikiliwa na Polisi huku majibu yakisubiriwa kutoka ofisi ya Mkemia
Mkuu kuthibitisha kama kweli unga aliokamatwa nao ni dawa za kulevya au
la.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert
Boaz, alisema mtu huyo alikamatwa unga huo ukiwa umehifadhiwa chini ya
begi lake la nguo, lakini mpaka sasa haijathibitika kuwa ni unga wa aina
gani.
Kamanda Boaz alisema wapo watu wanaofikiri kuwa
Kilimanjaro ni kivuko cha dawa za kulevya na kusisitiza kuwa Jeshi la
Polisi liko macho na kamwe hataruhusu heshima ya mkoa huo kuchafuliwa na
watu wachache.
“Kuna
watu wanadhani kuwa hapa kwetu ni uchochoro wa kupitisha madawa ya
kulevya na uchafu wa aina yoyote ile, hapa sio kivuko na kamwe
hatutaruhusu hilo. Chumu kwa sasa yuko chini ya mkono wa Polisi na
uchunguzi ukimalizika atafikishwa mahakamani,” alisema Boaz.
Wakati
huohuo, Jeshi la Polisi mkoani hapa limewakamata watu wawili wanaodaiwa
kumteka mtoto kwa madai ya kupata fidia kutoka kwa wazazi wa mtoto
huyo. Taarifa hizo zinasema kuwa mtoto huyo alitoweka nyumbani kwa bibi
yake Februari 27, majira ya saa 4 asubuhi na kwamba baada ya kufanyika
kwa operesheni maalumu kutoka kwa kikosi maalum cha Jeshi la Polisi,
alikutwa akiwa mikononi mwa mateka hao.
“Baada
ya kupata taarifa, tuliunda timu maalumu na kuwapata watekaji wakiwa
wilayani Rombo, mtego wetu ulinasa na kumkamata Nicholaus Lyimo akiwa
amejificha katika Kijiji cha Mashimba, Useri Rombo akiwa na mtoto
machakani, tulivyompekua tulikuta vyeti vyake vya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kisu,” alisema Boaz.
---
Habari imeandikwa na Fadhili Athumani, Moshi via gazeti la MTANZANIA
No comments:
Post a Comment