Wednesday, February 27, 2013

WANANCHI wilayani Rungwe wamefurahishwa na kitendo cha mwekezaji kukubali kujenga kiwanda cha kusindika gesi inayochimbwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya.


Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine Meela akimsikiliza mkurugenzi wa TOL Mcjohn Mbili akielezea hatua za mwisho za ujenzi wa kiwanda hicho cha gesi


Ndani ya kiwanda hicho cha gesi Rungwe


WANANCHI wilayani Rungwe wamefurahishwa na kitendo cha mwekezaji kukubali kujenga kiwanda cha kusindika gesi inayochimbwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Hata hivyo licha kiwanda hicho kujengwa Rungwe Serikali imesisitiza kuwa gesi hiyo ni mali ya watanzania wote na hakuna mwananchi wa Rungwe mwenye haki ya kuikatalia isisafirishwe kwenda maeneo mengine ya nchi.

 Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine Meela aliwahakikishia wananchi  kuwa watanufaika na gesi hiyo sambamba na watanzania wengine kwa kuwa gesi hiyo ni rasilimali ya taifa zima.

Meela ambaye alikuwa ametembelea eneo hilo kwa nia ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi hiyo aliwaeleza wananchi kuwa kiwanda hicho ni mali yao na watanzania wote ingawa kinasimamiwa na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Tanzania Oxgen Limited (TOL) kutoka nchini Kenya.

Alisema kuwa muwekezaji huyo amekubali kufuata sheria na taratibu zote za uwekezaji  pamoja na kushirikiana na jamii inayomzunguka eneo la mradi katika shughuli zote za maendeleo ya jamii.


“Tena jambo zuri zaidi ni kwamba Mwekezaji huyu amekubali kufuata sheria na taratibu za uwekezaji  pamoja na kutoa ushirikiano na jamii inayomzungumza ambao ndio ninyi wakazi wa hapa Ikama na Wana-Rungwe wote, hivyo tunao wajibu wa kukitunza kiwanda hiki kwa kuwa ni mali yetu,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Awali Mkurugenzi wa TOL, McJohn Mbiri, alisema kuwa kiwanda hicho  kitakuwa chachu ya maendeleo ya wananchi wa Rungwe mara baada ya kukamilika na kuanza kutumika, kwani kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wenye uwezo wa kufanya kazi.

Alisema kuwa watahakikisha wanatengeneza na kuboresha miundiombinu inayowazunguka wananchi hao ikiwemo  barabara, uboreshaji wa huduma ya Maji, kuwaingizia Umeme majumbani, kuwaboreshea vyumba vya madarasa katika shule za msingi na Sekondari pamoja na Zahanati ambayo tayari ilishaanza kujengwa.

“Niseme mbele ya wananchi wa Kijiji cha Ikama mkiwa  chini ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, hiki kiwanda siyo mali ya Wakenya ni mali ya wana-Rungwe, na tutashirikiana na wananchi katika shughuli za kijamii ambapo tayari tumeanza kujenga Zahanati kwaajili ya wanakijiji cha Ikama, baada ya kumaliza zahanati hiyo tutakarabati vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Isebe na Serokndari ya Itageta,” alisema na kuongeza:

“Pia tutahakikisha umeme unawafikia wananchi wote, miundombinu ya barabara ambayo ndiyo kiini cha Maendeleo itaboreshwa pamoja na kuboresha miundombinu ya maji ili wananchi mpate maji afi ya bombani,” alisema Mbiri.

Alisema kuwa gesi iliyopo wilayani hapo  ina uwezo wa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 300 bila ya kuonesha dalili zozote za kuisha hivyo wananchi wanatakiwa kujivunia uwepo wa kiwanda hicho kwani kitawanufaisha kwa kizazi kilichopo na kijacho.

Wakazi wa kijiji hicho cha Ikama nao hawakusita kuzungumzia matumani yao juu ya kuwapo kwa kiwanda hicho ambao walisema kuwa tayari wameanza kujionea matunda ya  kiwanda hicho ambapo ujenzi wa zahanati umeshaanza jambo walilodai kuwa itawapunguzia mzigo wa kusafiri mwendo mrefu kufuata matibabu vijiji jirani.

Daniel Mwandeko (60), alisema kuwa kitendo hicho cha kuwapo kiwanda hicho kinawafanya waamini kuwa wataboresha maisha yao kupitia miradi ya kijamii inayojengwa na kiwanda hicho kwenye maeneo yao.

“Binafsi nimefurahi kuona maendeleo yanayotokana na kiwanda hiki, kwanza wakati wakiwa katika ujenzi wa kiwanda chao tayari wameanza kutujengea Zahanati ya kijiji, hivyo tunaamini kwamba tutazidi kuboreshewa na miundombinu mbalimbali, ila tu naomba sana wazingatie suala la kutoa ajira kwa vijana wetu ambao ni wazalendo” alisema Mzee huyo.

No comments:

Post a Comment