Wednesday, February 27, 2013

MWANAFUNZI AFARIKI BAADA YA KUTUMBUKIA CHOONI:WAOMBA KUJENGEWA VYOO VIPYA

MIEZI michache baada ya wanafunzi wa Shule ya Sengerema Sekondari iliyopo Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, kufanya maandamano kisha kuharibu baadhi ya mali za shule hiyo wakidai kujengewa vyoo shuleni hapo, mwanafunzi mmoja, Yunis Kajiti aliyekuwa anasoma Kidato cha Sita, amefariki dunia baada ya kutumbukia chooni shuleni hapo.

Tukio hilo limetokea leo alfajiri, baada ya mwanafunzi huyo aliyekuwa anatajarajia kumaliza mtihani wake wa mwisho hii leo, alipotoka kwenye bweni kisha kwenda kwenye choo cha shule hiyo, ambapo inadaiwa akiwa anajisaidia ghafla mbao za choo hicho zilivunjika kisha kutumbukia ndani kwenye vinyesi.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Sanane John aliiambia FikraPevu kwamba: 
Alfajiri hiyo kuna mwanafunzi mwenzetu alikuja akaniambia kuna mtu ametumbukia chooni. Baada ya hapo nikajifunga kamba kiunoni na nikatumbukia kwenye shimo hilo na kuanza kumtafuta kwa kugusa gusa na fimbo, ndipo nikakutana naye na nikamshika na kumbemba huku wenzangu wakinivuta kisha kumtoa nje.
Mkuu wa shule hiyo aliyetajwa kwa kwa jina moja Kahema na Ofisa Elimu Sekondari wa wilaya ya Sengerema, Venance Mwizarubi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku msemaji wa Mganga mkuu wa hospitali Teule ya wilaya ya Sengerema, aliyejitambulisha kwa jina moja la Dk Muguta naye alikiri kupokea mwili wa mwanafunzi huyo akiwa amefariki dunia.
 
Habari imeandikwa na Sitta Tumma, Mwanza via FikraPevu

No comments:

Post a Comment