Wednesday, February 27, 2013

Mufti Simba atengua nafasi ya Sheikh Mkuu Semwali wa Morogoro


Sheikh Mkuu na Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, ametengua nafasi ya Shekhe Mkuu mkoani Morogoro, Yahya Semwali akidaiwa kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu mkoani humo.

Katika barua yake kwa Shekhe Semwali yenye namba MK/BR/UL/03/04/79 ya Februari 19 mwaka huu, Mufti Simba alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Baraza la Ulamaa Taifa hivyo anatakiwa kukabidhi ofisi.

Kutokana na uamuzi wa baraza hilo, Mufti Simba amemteua Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaaban kukaimu nafasi hiyo kwa barua yenye namba MK/BR/UL/03/04/81 ya Februari 20 mwaka huu na kusisitiza kuwa, nafsi hiyo inapaswa kujazwa ndani ya siku 90 kwa kufanya uchaguzi mwingine.

“Waumini wa Kiislamu mkoani Morogoro wapewe fursa ya kuchagua Sheikh mwingine wa Mkoa,” ilisema barua hiyo.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na viongozi mbalimbali wa BAKWATA mkoani humo akiwemo Sheikh
Semwali aliyeondolewa madrakani ambaye alisema madai yaliyotolewa dhidi yake si sahihi na yameegemea upande
mmoja yakisukumwa na hisia zaidi.

Alisema kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kunatokana na hisia za kuunga mkono msimamo wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda jambo ambalohalina ukweli.

Sheikh Semwali alisema:
Hisia nyingine zilizojionesha ni kitendo cha mimi kwenda ibada ya Hijja kupitia taasisi nyingine tofauti na Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), pamoja na uamuzi wangu wa kutengua uchaguzi wa baraza hili ngazi ya kata, wilayani Gairo.

Uchaguzi huu ulifanyika kinyime na utaratibu bila ya ngazi husika kama BAKWATA Wilaya na Mkoa kuwa na taarifa, hili ndio lililomsukuma Mufti Simba kufikia maamuzi haya japo baraza hili Mkoa lina taarifa za ukikukwaji husika lakini bado aliendelea kukaa kimya.
Kuhusu madai ya kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu, Sheikh Semwali alisema hivi sasa katika Wilaya zote kuna miradi ya maendeleo kama ule wa Wilaya ya Ulanga ambako kuna ujenzi wa vyumba vya maduka 14.

Pia kuna mchakato wa upatikanaji ekari 20 kwa ajili ya upandaji miti ya matunda ambapo hivi sasa walikuwa kwenye hatua za mwisho kupata ekari nyingine 600.

Alisema Wilaya ya Morogoro Vijijini kuna vyumba vitano vya maduka, Mvomero vyumba vinne vya madrasa na Kilombero vyumba vitano vya biashara ambapo maendeleo hayo  yametokana na juhudi zake.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Masheikh mkoani humo, ambalo lilikaa hivi karibuni kupitia maamuzi hayo, Sheikh Shaaban Nyoni, alisema uamuzi wa Mufti Simba amekiuka Katiba ya BAKWATA.
Shekhe Semwali alichaguliwa hakuteuliwa hivuyo kama alikuwa na tatizo, wao kama baraza ndio waliopaswa kuwasilisha tatizo lao kwa Mufti Simba si vinginevyo.

Halmashauri ya BAKWATA Mkoa inatarajia kukutana kesho (leo), ili kujadili uamuzi huu na baadaye kikao cha Mashekhe wote wa Wilaya na Mkoa, watakaa kujadili na kutoa msimamo.
Imam wa Msikiti wa Al Aqswaa wa Mazimbu, mkoani humo, Sheikh Mohamed Msoma ambaye ni mjumbe wa Baraza la Masheikh, alisema si sahihi Mufti Simba kumuondoa Sheikh Semwali katika nafasi yake.
 
Imeandikwa na Aziz Msuya, Morogoro via gazeti la MAJIRA

No comments:

Post a Comment