PADRI
wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili lililoko Mji Mkongwe
Zanzibar, Evaristus Mushi ameuawa kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana jana asubuhi wakati akielekea kanisani kuendesha ibada.
Tukio hilo limetokea majira ya saa moja asubuhi
wakati padri huyo akijitayarisha kwenda kuongoza ibada ya Jumapili
katika Kanisa la Mtoni nje kidogo na Mji wa Zanzibar.
Hilo ni tukio la pili kutokea kwa padri kupigwa
risasi Zanzibar baada ya Desemba 26, mwaka jana Padri Ambros Mkenda wa
Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje
ya nyumba yake saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.
Akizungumzia tukio la jana, Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini (IGP), Said Mwema pamoja na kuthibitisha, alisema ametuma
timu ya wapelelezi kwenda Zanzibar kuchunguza kwa undani kuhusu tukio
hilo.
“Watu wasiojulikana wamempiga risasi Padri Mushi,
na baada ya tukio alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja na kufariki dunia.
Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema IGP Mwema.
Alisema hadi sasa watu watatu
wameshakamatwa kuhusiana na tukio hilo na msako mkali unaendelea na
kuchunguza tukio zima. IGP Mwema alisema ametuma timu Zanzibar
itakayoongozwa na Manaibu Kamishna wa Polisi wawili ambao ni Samson
Kasalla na Peter Kivuyo wakiwa pamoja na Kamanda wa Operesheni wa jeshi
hilo, Simon Sirro.
“Tumekuwa tukifuatilia nyendo hizi na hivi sasa
tutapambana na wahalifu ipasavyo, vurugu zozote zile lazima tupambane
nazo ipasavyo,” alisema Mwema na kuongeza: “Kama kwenye tukio hili
kutakuwa na masuala ya kigaidi nayo tutachunguza.” Alisema
watawatafuta kwa udi na uvumba wale wote wanaochochea au kufadhili
yanayotokea kwa kuwa wanachokifanya ni uhalifu. Mwili wa padri huyo sasa
umehifadhiwa katika mochwari ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Katika
Kanisa la Minara Miwili, Mji Mkongwe waumini walikusanyika wakionyesha
hali ya kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kifo hicho cha
ghafla. Wakizungumza kwa masikitiko waumini hao wamesema hawakuwa
wakijua chochote kilichotokea hadi hapo walipofika katika kanisa kwa
ajili ya kufanya ibada. “Tumetoka nyumbani tukiwa na matumaini
makubwa ya kufanya ibada zetu kwa amani, lakini tulipofika hapa
tumepokea taarifa kuwa padri wetu amepigwa risasi, jamani Mungu hiki ni
nini, mbona Zanzibar imegeuka kuwa nchi isiyo na amani, vipi tutaishi
katika hali kama hii ya kuhofu na wasiwasi...Mungu tusaidie waja wako
sisi,” alisema mama mmoja huku akilia kwa majonzi.” Mashuhuda Walioshuhudia
tukio hilo wanasema kawaida Padri Mushi huwa anakwenda kusalisha katika
Kanisa la Mtoni na kwamba jana, baada ya kufika kanisani hapo wakati
akitaka kuegesha gari lake walifika watu kwenye gari lake na kumfyatulia
risasi na kisha kukimbia kusikojulikana. Makamu Askofu wa kanisa
hilo Zanzibar, John Mfoi alisema kuwa watu waliompiga risasi Padri Mushi
walikuwa wapo kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia
kwa nyuma wakati akieleke kanisani. “Baada ya kufika karibu na kanisa
alipigwa risasi na gari kupoteza mwelekeo kisha kwenda kuonga
nyumba,”alisema na kuongeza: “Uchunguzi wa hospitali umegundua alipigwa
risasi tatu mbili zimetolewa kichwani na nyingine haijulikani iliko.” Matukio
kama hayo ya kihalifu yamekuwa yakitokea mara kwa mara Zanzibar ambapo
katika kipindi cha mwezi mmoja watu watatu walipigwa risasi maeneo ya
Bububu na Mbweni, lakini hii ni mara ya pili kwa padri kupigwa risasi
katika historia ya Zanzibar. TEC wasikitika Makamu wa Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Severin Niwemugizi alisema
tukio hilo linatia mashaka kwa kuwa mauaji hayo yanaonyesha kuwa ni ya
kupanga. “Nimepata taarifa kwamba kuna mwenzetu ameuawa huko, lakini
inaonekana ni mauaji ya kupangwa kwa kadiri ya hamasa ambazo zinatolewa
na dini fulani, kwani waliwahi kusema hatutaifurahia Pasaka, nadhani
ndiyo wanatekeleza hilo,” alisema Niwemugizi.
Alisema tukio hilo ni la kuogopesha na linaonyesha
nchi inakoelekea si kuzuri kwa kuwa kikundi fulani kimeachiwa na
kinafanya mauaji na kuwatendea maovu wengine lakini viongozi wamekaa
kimya.
“Hii ni ishara mbaya kwani Serikali ipo hivyo
tunahitaji kauli yao kuhusu haya mambo, kwa kweli nina mashaka na
yanayotokea ili yasije yakatufikisha kwenye mauaji ya kimbari
yaliyotokea Rwanda,”alisema Niwemugizi.
JK atuma rambirambi Rais Jakaya Kikwete alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi.
“Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu
zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa
haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata
ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”
|
No comments:
Post a Comment