Tuesday, September 4, 2012

TCJ YALAANI MAUAJI YA DAUDI MWANGOSI, YATOA WITO WANAHABARI KUTOANDIKA HABARI ZA KISIASA

 

Sisi kama chama cha wandishi wa habari wasiokuwa na ajira za kudumu katika vyombo mbalimbali vya habari nchini na wale wa kujitegemea (TCJ), tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za mauaji ya kikatili dhidi ya mwandishi wa habari wa kituo cha Channel 10 Daudi Mwangosi kutoka Iringa

Marehemu Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Club ya waandishi wa habari (IPC) Iringa aliuwawa na bomu wakati akitekeleza wajibu wake kikazi katikati ya mvutano wa kisiasa kati ya Polisi na wafuasi wa CHADEMA, Septemba 2 Mwaka 2012.

Licha ya taarifa za awali kudai kuwa Mwandishi huyo aliuawa na bomu lililolipuliwa na Polisi bado taarifa hazijawekwa wazi kilichotekea hadi kufikia hatua hiyo ndio maana Polisi na jukwaa la Wahariri, pamoja na baraza la habari wameunda tume kuchukunguza tukio hilo lenye kufedhehesha taifa letu.

Wakati taasisi hizo zinachukua hatua ya kuchunguza tukio hilo, tunatoa mwito kwa wadau wa habari na waadishi wenyewe kutumia kifo cha Mwangosi kama changamoto ya kushinikiza wandishi wa habari hususani wale wasiokuwa na ajira ya kudumu (Correspondent) wawekewe bima ya maisha wanapokuwa kwenye mikutano ya kisiasa au maandamano.

Ikumbukwe kuwa Tanzania ina Waandishi wa Habari wasiopungua 4000 na kati yao asilimia 75 ya waandishi hao ni waandishi wasiokuwa na ajira za kudumu yaani (FREELANCES AND CORRESPONDENT).

Hivyo wengi wao kwa kutokuwa na ajira ndiyo wamekuwa wakitumwa na vyombo vyao kwenda kwenye matukio ya hatari kama hayo na hata pale linapotokea tukio baya linaloweza kusababisha kifo mara nyingi vyombo vyao huwaruka kuwa sio wafanyakazi wao bali ni wawakilishi tu.

Wakati MCT pamoja na TEF wanapojenga hoja ya wanahabari kususia kuandika habari za jeshi la Polisi sisi kama TCJ tunakwenda mbali zaidi na kuwataka wanahabari wagome kujitokeza kwenye mikutano ya kisiasa hadi watakapohakikishiwa bima ya maisha endapo machafuko yatatokea.

Tunao ushahidi jinsi wanahabari wanavyopata taabu pindi wanapopata ajali wakiwa kazini, wapo ambao waligeuka mzigo wa familia baada ya kutelekezwa na vyombo wanavyofanyia kazi eti kwa madai kuwa alikuwa analipwa kwa stori.

Watu wenye jukumu la kuwakea bima ya maisha ni wadau wote wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wanasiasa wanaowaalika wandishi kwenye mikutano au ziara za kukagua shughuli za maendeleo.

Mwandishi ambaye alikuwa hajaajiriwa anapoumuia au kufariki haki zake hupotea kwasababu hana, Bima ya Afya, wala kadi ya NSSF hivyo ni wakati muafaka sasa kwa wadau wa habari kuitisha mjadala wa wazi ili kuona namna ya kuwalinda na kuwajali wandishi wanapokuwa kwenye machafuko.

TCJ tunashauri tamko la kususia habari za Polisi lipimwe upya tuone kama litawaathiri kwa namna yoyote Polisi, huku tukijiuliza kuwa kesho mfuasi wa chama cha Siasa atakapomshambulia mwandishi wa habari kwenye mavuguvugu yao je wanahabari tutasusia habari za chama hicho?

Aidha wakati tukilaani tukio hilo ambalo Waziri wa Mambo ya ndani amethibitisha kuwa limetokea baada ya askari kufyatua bomu bila kutumia utalaam, tunaamini kuwa viongozi wa jeshi la Polisi watawajibika kwa uzembe huo huku tukiwasihi Polisi warejelee kauli mbiu yao ya ulinzi shirikishi kutowapiga wandishi wakiwa kazini kwa lengo la kuwatisha wasiende kuandika maouvu wanayoyafanya.

Kwa mauaji hayo yaliyotokea Iringa tunawaomba wadau wote wa habari tuweze kushikamana kuhakikisha muuji anakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili jamii iweze kurejesha imani kwa dola yao, vingenevyo usalama wa wandishi utakuwa taabani.

Aidha tunatoa wito kwa mara nyingine serikali iwape askari Polisi mafunzo ya kushirikiana na wanahabari wakati wa kukabiliana na machafuko, kwani tunapoelekea bila semina elekezi huenda wanahabari wengi wakaumizwa hasa nyakati za uchaguzi hivyo ni matumaini yetu kuwa mauaji ya Iringa yatakuwa yametufungua macho
…………………………….
Mobini Sarya
Mwenyekiti-TCJ