Jembe Mrisho Khalfan
Ngassa ameuzwa Simba kwa dau la Sh. Milioni 25 mchana wa leo.
Habari
kutoka Azam, ambazo MAASINDA imezipata kutoka klabu hiyo, zimesema
kwamba Simba wamelipa fedha hizo na wamesainiwa fomu za uhamisho na sasa Mrisho
anafuata nyayo za baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC
1991/1992.
Azam ilifikia
uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo aliyetoka yanga
miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili
katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo,
ni wa mzee Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho
akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote,
haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa
amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga
miaka miwili iliyoipita kwa dau la Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja
kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa Simba kumsajili, kuna hatari
yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa Wekundu wa Msimbazi.
Mapema leo
mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana alifukuzwa katika
klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo,
kumpanga Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame.
Habari ambazo BIN
ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha
pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha
Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha
kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema
kwamba, mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS
Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha
mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la
ushindi.
Lakini Stewart
katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi
na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni
asipangwe tena.
Katika fainali,
Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa
kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na
mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia
alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa
alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda
2-0.
Mbali na
Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ pia yuko katika wakati mgumu na jana
inadaiwa alionekana akilia wakati anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam,
akiuliza ni lipi kosa lake.
Sure Boy,
ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’
jana hajafanya mazoezi na leo pia, naye pia akituhumiwa kucheza kinazi katika
mechi dhidi ya Yanga.
Stewart anakuwa
kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos,
Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.