WATEJA zaidi ya 50 wa Benki ya
Uchumi Commercial Bank Ltd (UCB) ya Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT) wanasakwa na polisi kufuatia wizi wa karibu Sh250
milioni.
Vyanzo vya kuaminika vilidokeza kuwa
ingawa taarifa zilizofunguliwa polisi na menejimenti ya UCB zinaonyesha kiasi
kilichoibwa ni Sh224 milioni, lakini kinaweza kufikia Sh250 milioni kadri
uchunguzi unavyoendelea.
Benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005
baada ya kupatiwa leseni namba CBA 00031 na Benki kuu ya Tanzania (BoT),
inamilikiwa na Watanzania wapatao 330,000 ambao ni waumini wa dayosisi hiyo.
Habari za uhakika zilizolifikia
Mwananchi zilisema wizi huo ulifanyika baada ya kuparanganyika kwa mfumo wa
kompyuta uliounganishwa na mashine za ATM.
Taarifa nyingine zilisema wizi huo
ulitokana na baadhi ya wateja kuusoma mfumo wa kompyuta hiyo na kugundua kuwa
kuna nyakati za usiku huchanganyikiwa na kutoa salio lisilo sahihi la wateja.
“Kilichotokea ni kuwa kuna watu
walivujisha siri kuwa nyakati za usiku sana ukichomeka kadi kwenye hiyo ATM
inatoa pesa hovyo hovyo hata kama hauna salio la kutosha”kilidokeza chanzo
chetu.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa
wateja wa benki hiyo wapatao 50 walijihusisha na wizi wa fedha hizo kupitia ATM
hiyo na tayari polisi imeanzisha uchunguzi maalumu wa kuwasaka.
Habari hizo zimedai kuwa baada ya
kugundulika kwa dosari katika mfumo huo wa kompyuta za ATM katika benki hiyo,
baadhi ya wateja walianzisha kuchukua fedha muda mfumo huo unapoharibika.
“Sio pesa zilizoibwa mara moja
hapana yaani unakuta leo anatoa 500,000 kesho hivyo hivyo na ilikuwa ni wateja
tofauti tofauti waliokuwa wamegundua siri hiyo”alidokeza mtumishi mmoja wa UCB.
Baadhi ya wanasheria walidai zipo
changamoto nyingi katika kesi za aina hiyo hasa katika kuthibitisha kama wakati
mtuhumiwa anatoa fedha hizo katika ATM,alikuwa amekula njama ya kutenda kosa
hilo.
Meneja mkuu wa Benki hiyo, Angela
Moshi alipoulizwa alikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini akasema hakuwa katika
nafasi nzuri ya kulielezea kwa vile alikuwa akielekea kanisani kwa ajili ya ibada.
"Naomba uje kesho
(leo)tutazugumza vizuri tu juu ya hilo jambo nitakupa taarifa vizuri tu unajua
leo ni siku ya ibada na sasa hivi naingia kanisani kwa ajili ya
ibada"alisisitiza Meneja mkuu huyo jana.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kilimanjaro,Robert Boaz alipoulizwa na gazeti hili juzi alisema“ni
kweli hilo tukio lipo kwa maana ya wateja ‘wame overdraw’ (wametoa zaidi)
kutoka kwenye akaunti zao na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea”alisema Kamanda
Boaz.
|