Msanii
wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia
kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7,
2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mazishi
ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu,
mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa
fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya
filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila
mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika
tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya
milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.
RATIBA
Mwili
wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya
Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa
Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni
ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya
watu wote kumuaga.
Wito
unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi,
wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi
ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.
Saa 3:30 asubuhi,
mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na
mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao
kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Mohamed Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa
ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka
kwa watu mbalimbali.
Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga
Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati
wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya
Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya
Kinondoni kuelekea makaburini.
Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu
watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili
kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani
aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake
ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.
K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI